Israel iliwaua waandishi habari 18 wa Kipalestina mwezi Novemba
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119878-israel_iliwaua_waandishi_habari_18_wa_kipalestina_mwezi_novemba
Takriban wafanyakazi 18 wa vyombo vya habari waliuawa mwezi Novemba katika mashambulizi ya nchi kavu na ya anga ya jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-12-08T10:38:08+00:00 )
Dec 08, 2024 10:38 UTC
  • Israel iliwaua waandishi habari 18 wa Kipalestina mwezi Novemba

Takriban wafanyakazi 18 wa vyombo vya habari waliuawa mwezi Novemba katika mashambulizi ya nchi kavu na ya anga ya jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.

Hayo yamedokezwa na Kituo cha Palestina cha Maendeleo na Uhuru wa Vyombo vya Habari (MADA) ambacho kimesema kwamba utawala wa Israel unalenga kwa makusudi waandishi wa habari ili kukandamiza utangazaji wa jinai zake za kivita.

MADA imeripoti kuwa vikosi vya Israel vilifanya ukiukaji 65 dhidi ya waandishi wa habari katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu na Gaza katika kipindi kilichotajwa.

Mamlaka za Palestina zinasema waandishi wa habari 192 wameuawa katika mashambulizi ya Israel katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita vya umwagaji damu vya Israel dhidi ya eneo la pwani lililozingirwa mwezi Oktoba mwaka jana.

Ikiungwa mkono na Marekani na washirika wake wa Magharibi, Israel ilianzisha vita dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023, baada ya harakati ya muqawama wa Palestina Hamas kutekeleza Operesheni ya Kimbunga cha ya Al-Aqsa dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel ili kukabiliana na jinai zake za miongo kadhaa dhidi ya Wapalestina.

Mashambulizi hayo ya mauaji ya kimbari ya utawala huo kwenye kanda wa Gaza hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina 44,664 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kujeruhi wengine 105,976. Maelfu zaidi pia hawapo na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.

Tarehe 21 Novemba, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wa zamani wa masuala ya kijeshi Yoav Gallant kwa uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.

Israel pia inakabiliwa na kesi ya mauaji ya halaiki katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa vita vyake vya mauaji ya umati dhidi ya Gaza.