Bashar al-Assad na familia yake wapewa hifadhi Russia
Kanali ya Kwanza ya Televisheni ya Russia imeripoti ikiinukuu ikulu ya nchi hiyo Kremlin kwamba aliyekuwa Rais wa Syria Bashar al-Assad na wanafamilia wake wako Moscow.
Kanali hiyo ya Televisheni imesisitiza kuwa, Bashar al-Assad amewasili Moscow pamoja na familia yake na kupewa hifadhi.
Kufuatia tetesi nyingi kuhusu mahali alipo Bashar al-Assad, chanzo kutoka Ikulu ya Kremlin kilitangaza jioni ya jana (Jumapili) kwamba Bashar al-Assad aliwasili Moscow na familia yake na kwamba, serikali ya Russia imewapa hifadhi.
Habari za kuwepo kwa Assad nchini Russia zimetangazwa baada ya Shirika la Habari la Uingereza Reuters kudai kuwa huenda ndege iliyombeba "Bashar Assad" ilianguka wakati ikijaribu kuondoka Syria na kiongozi huyo wa zamani wa Syria kuuawa.
Serikali ya Syria ilianguka mapema jana Jumapili katika mwisho wa kushangaza kwa uongozi wa miaka 24 wa Rais Bashar al-Assad katika nchi hiyo ya Kiarabu baada ya kundi la wanamgambo wa Hay’at Tahrir al-Sham (HTS) kuvamia na kuuteka mji mkuu Damascus.
Katika taarifa ya Jumapili asubuhi, wanamgambo wa HTS walitangaza kuwa wameuteka mji mkuu, na kuthibitisha ripoti za kuanguka kwa serikali ya Assad.