Wanajeshi 4 wa Israel wauawa kwenye handaki kusini mwa Lebanon
Jeshi la Israel limekiri leo Jumatatu kuwa wanajeshi wake wanne wameuawa kusini mwa Lebanon, likiwa ni tukio la kwanza la aina yake tangu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano siku 12 zilizopita.
Jeshi la Israel limethibitisha kuwa wanajeshi hao wanne wameuawa wakati handaki walimokuwa lilipoporomoka baada ya kulipuliwa.
Limeongeza kuwa askari hao wanne walikuwa wa kikosi kimoja na "waliuawa wakati wa mapigano" jana Jumapili, bila kutoa maelezo zaidi.
Kwa upande wake, gazeti la Yedioth Ahronoth, limeripoti kuwa wanajeshi hao wanne wa Israel ndio wa kwanza kuuawa nchini Lebanon tangu bada ya makubaliano ya kusitishwa mapigano.
Licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano, jeshi la utawala ghasibu wa Israel limekuwa likishambulia mara kwa mara maeneo ya kusini mwa lebanon na kuua raia wasio na hatia.
Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kwamba mashambulizi ya Israel katika vijiji viwili vya kusini mwa nchi hiyo yameua watu sita, katika changamoto mpya inayoteteresha makubaliano ya usitishaji vita kati ya utawala huo haramu na harakati ya Hizbullah, ambayo yalianza kutekelezwa yapata wiki mbili zilizopita.