Sababu za ndani za kuanguka kwa serikali ya Bashar Assad
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119976-sababu_za_ndani_za_kuanguka_kwa_serikali_ya_bashar_assad
Baada ya kifo cha Rais Hafez Assad mwaka 2000, mwanawe Bashar Assad alichukua mamlaka nchini Syria kubakia madarakani nchini Syria kwa miaka 24.
(last modified 2024-12-10T10:16:23+00:00 )
Dec 10, 2024 10:16 UTC
  • Sababu za ndani za kuanguka kwa serikali ya Bashar Assad

Baada ya kifo cha Rais Hafez Assad mwaka 2000, mwanawe Bashar Assad alichukua mamlaka nchini Syria kubakia madarakani nchini Syria kwa miaka 24.

Kwa msingi huo kiujumla familia ya Assad ilikuwa madarakani katika nchi hiyo kwa miaka 54. Baada ya serikali ya Bashar Assad kuanguka Jumapili ya juzi, kivitendo mamlaka na hatamu za uongozi za familia ya Assad huko Syria zimefikia tamati na nchi hiyo imo mbioni kufungua ukurasa mpya wa uongozi. Bila shaka kuna sababu za ndani na za nje zilizopelekea kuanguka serikali ya Bashar al-Assad na kumfanya aihame nchi na kuelekea Moscow.

Weledi wa mambo wanataja sababu kadhaa za ndani zilizopelekea kuanguka utawala wa Assad.

Moja ya sababu muhimu za kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad nchini Syria ni kuzidi kwa matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo na athari zake katika uungaji mkono wa watu kwa serikali. Kufuatia vita vya miaka saba dhidi ya magaidi na kuharibiwa miundombinu ya Syria na pia kupoteza vyanzo vyake vya mapato na kuwekewa vikwazo na serikali ya Marekani, matatizo ya kiuchumi ya nchi hiyo yalishadidi na kuongezeka maradufu.

Mfumuko wa bei ambao haujawahi kushuhudiwa na kufanya maisha kuwa magumu kwa watu kulipunguza sana uwezo wao wa kustahimili matatizo na kusababisha utawala wa Bashar al-Assad kupoteza uungaji mkono wake kutoka kwa wananchi.

Bashar al-Assad Rais wa zamani wa Syria

 

Jambo la pili muhimu linalotajwa na wajuzi wa mambo kwamba, limechangia kuanguka kwa utawala wa Syria ni nafasi ya jeshi la nchi hiyo. Katika mwaka 2011 hadi 2017, jeshi la Syria liliunga mkono kwa dhati umoja wa ardhi ya nchi hiyo na lilikuwa na nafasi kubwa katika mapambano dhidi ya magaidi. Hata hivyo, jeshi la Syria halikuweza kukabiliana na makundi ya upinzani katika duru mpya ya harakati na halikuwa na nia ya kujihami dhidi ya makundi hayo.

Matatizo ya kiuchumi pia yaliathiri jeshi la Syria na mishahara yao midogo ikilinganishwa na mfumuko wa bei ambao ulifanya suala la kutaka kubadilishwa serikali kutokuwa muhimu kwao.

Abdelreza Faraji Rad, profesa wa jiopilitiki anasema kuhusiana na hili: "Wapinzani wa Syria waliweza kufika haraka Aleppo kutoka Idlib, na kisha wakaiteka miji mingine kuelekea kusini mwa Syria moja baada ya nyingine na kutokuweko harakati na mapambano ya jeshi la Syria katika kukabiliana wapinzani bila shaka ilikuwa sababu muhimu ya kusonga mbele wapinzani.

Mfumuko wa bei mbaya na wa kutisha na usiozuilika nchini Syria ulisababisha hata wanajeshi kutokuwa na dhamira ya kukabiliana na upinzani wenye silaha; kwa sababu mishahara ya askari haikuwa ikilipwa kwa wakati au kwa sababu mfumuko wa bei ulikuwa mkubwa kiasi kwamba kimsingi nao walikuwa wakikabiliwa na matatizo mengi katika kukidhi mahitaji yao ya kila siku ya maisha.

Wapiganaji wa makuundi ya upinzani Syria

 

Jambo la tatu muhimu na moja ya sababu za ndani zilizopelekea kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad nchini Syria ni kwamba, baada ya kushindwa kwa magaidi mwaka 2017 na katika kipindi cha miaka 7 iliyopita, Bashar al-Assad hakufanya juhudi zozote za kurekebisha muundo wa madaraka wa Syria, kwani wakosoaji na makundi ya upinzani ya utawala wa Syria waliendelea kubakia mbali na nje ya mamlaka na uongozi wa nchi hiyo.

Suala hili pia lilisababisha makundi ya upinzani kuungana na makundi ya kigaidi na kuunda muungano dhidi ya utawala wa Syria katika miezi iliyopita na kuchukua hatua ya kuupindua utawala wa Assad nchini Syria.