Waziri Mkuu wa Iraq aonya kuhusu mashambulizi dhidi ya Syria
Waziri Mkuu wa Iraq, Mohammed Shia' al-Sudani amesisitiza umuhimu wa kuzuia uvamizi wowote katika maeneo ya Syria unaofanywa na upande wowote, akionya kwamba vitendo hivyo vinatishia moja kwa moja usalama na utulivu katika eneo la Asia Magharibi.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeanzisha mashambulizi mapema Jumamosi yakilenga maeneo ya kijeshi mjini Damascus na mashambani mwake, katika mashambulizi ya hivi punde tangu wanamgambo wamuangushe Bashar al-Assad karibu wiki moja iliyopita.
Al-Sudani siku ya Ijumaa alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken mjini Baghdad ambapo walijadili uhusiano wa pande mbili kati ya Iraq na Marekani, njia za kuimarisha ushirikiano wa pande zote, na hali katika eneo hilo, hasa yanayoendelea nchini Syria.
Waziri Mkuu wa Iraq amesisitiza "msimamo wa nchi yake wa kuunga mkono Syria katika awamu hii muhimu na kusisitiza umuhimu wa kuwasaidia Wasyria katika kujenga upya nchi yao na kutatua changamoto zinazoweza kuathiri amani yao ya kiraia."
Zaidi ya wanajeshi 4,000 wa jeshi la Syria wamevuka mpaka na kuingia Iraq tangu wanamgambo waiteka Damascus, maafisa wamesema. Mkutano na Blinken pia ulizungumzia hali ya Gaza, na kusisitiza haja ya kuendelea na juhudi za kumaliza vita vya mauaji ya halaiki na kuhakikisha hatua zote muhimu za kuimarisha usitishaji vita nchini Lebanon.
Tangu kuanguka kwa Assad, Israel imetekeleza mamia ya mashambulizi dhidi ya maeneo ya kijeshi ya Syria, ikilenga kila kitu kuanzia maghala ya silaha za kemikali hadi ulinzi wa anga.