UNRWA: Jinai za Jeshi la Israel Gaza zinaumiza
Operesheni za kijeshi zinazoendeshwa na jeshi la utawala ghasibu wa Israel huko Gaza zimeendelea kuwasababishia matatizo watoto wa Kipalestina na familia zao, huku idadi ya vifo vikiongozeka.
Afisa Mwandamizi wa Masuala ya Dharura wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina, UNRWA, Loiuse Wateridge amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kutokea eneo la kati la Ukanda wa Gaza.
Afisa huyo wa UNRWA amesema: “Vyombo vya habari hapa vimeripoti kuwa Alhamisi usiku, watu 30 waliuawa kwenye eneo hili kutokana na mashambulizi. Tumeona picha za kutisha kutoka eneo hilo. Kuna wazazi wanatafuta watoto wao, watoto waliojaa damu mwilini wakitafuta wazazi wao, majeruhi lukuki wameripotiwa, na watu bado wamefukiwa kwenye vifusi."
Mashambulizi hayo yamekuja siku moja baada ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio la kutaka sitisho la haraka la mapigano Gaza bila masharti yoyote.
Bi. Wateridge ameelezea hali ya sasa kama “ya kuumiza,” akisema maumivu ya kila siku na machungu yamekuwa mambo ya kawaida kwa wapalestina waishio Ukanda wa Gaza.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza tarehe 7 Oktoba 2023 na hadi sasa yamesababisha vifo vya Wapalestina wasiopungua 45,00 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine zaidi ya 105,800. Maelfu zaidi pia wametoweka na inakisiwa kuwa wamekufa chini ya vifusi.