Mahmoud Abbas: Tatizo letu si Iran, ni Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120156-mahmoud_abbas_tatizo_letu_si_iran_ni_israel
Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameliambia gazeti moja la Italia kwamba tatizo la Palestina si Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali ni utawala wa Kizayuni wa Israel.
(last modified 2024-12-14T23:38:00+00:00 )
Dec 14, 2024 23:38 UTC
  • Mahmoud Abbas: Tatizo letu si Iran, ni Israel

Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ameliambia gazeti moja la Italia kwamba tatizo la Palestina si Jamhuri ya Kiislamu ya Iran bali ni utawala wa Kizayuni wa Israel.

Mahmoud Abbas ambaye ni maarufu kwa jina la Abou Mazin amesema hayo katika mahojiano hayo ambayo yameripotiwa pia na Shirika la Habari la Fars na kuongeza kuwa: "Nimezungumza na Trump kwa simu kuhusu amani ya kudumu ya Mashariki ya Kati."

Mkuu huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina vilevile ameliambia gazeti hilo la Corriere della Sera la Italia wakati wa ziara yake nchini humo kwamba tatizo ni Israel, si Iran. 

Amesema: Mashambulizi ya jeshi la Israel yameshaua na kujeruhi zaidi ya Wapalestina laki moja na 50,000 na ametoa mwito wa kuweko jitihada kubwa zaidi za kimataifa za kuilazimishwa Israel ikomeshe jinai zake huko Ghaza. 

Aidha amesema: "Wapalestina milioni 15 wana haki ya kuishi kwa usalama, utulivu na ustawi katika nchi yao wenyewe, yaani Palestina huku mji mkuu wake ukiwa ni Baytul Muqaddas."

Akizungumzia mkutano wake na Papa Francis, Mkuu huyo wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, Wakristo nao wanapaswa kuliunga mkono taifa la Palestina na mapambano yake mbele ya jinai za Wazayuni na kusisitiza kuwa, Israel iliripua kanisa la kihistoria la San Porfirios katika Ukanda wa Ghaza na kuua Wakristo 19 kwa mpigo, bila ya kujali kuwa hao ni Wakristo na hilo ni eneo lao la ibada.