Israel yaendeleza mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza, Palestina
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120174-israel_yaendeleza_mauaji_ya_waandishi_wa_habari_huko_gaza_palestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza mauaji dhidi ya waandishi wa habari kwa kuua mwandishi mwingine wa habari wa Kipalestina katika shambulio la anga huko Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-12-15T06:37:20+00:00 )
Dec 15, 2024 06:37 UTC
  • Israel yaendeleza mauaji ya waandishi wa habari huko Gaza, Palestina

Utawala wa Kizayuni wa Israel umeendeleza mauaji dhidi ya waandishi wa habari kwa kuua mwandishi mwingine wa habari wa Kipalestina katika shambulio la anga huko Ukanda wa Gaza.

Mauaji hayo yanaifanya idadi ya waandishi habari waliouawa tangu kuanza kwa mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya watu wa Gaza kufikia 195.

Taarifa ya Jukwaa la Waandishi wa Habari wa Palestina imesema kwamba Mohammed Ba’lousha, mwandishi wa idhaa ya kibinafsi ya al-Mash-had ya Lebanon na Dubai, aliuawa jana Jumamosi wakati ndege isiyo na rubani ya Israel iliposhambulia eneo la Gaza.

Shirika hilo lisilo la kiserikali limelaani "ukimya wa jamii ya kimataifa na kushindwa kuwalinda waandishi wa habari wa Palestina na na kwamba inapaswa kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao ya kitaaluma kwa mujibu wa sheria za kimataifa na mikataba ya kibinadamu."

Ndege isiyo na rubani ya Israel ililenga nyumba ya Ba’lousha kwenye Mtaa wa Ahmed Yassin katika kitongoji cha al-Saftawi, kaskazini mwa Jiji la Gaza.

Mohammed Ba’lousha

Alkhamisi iliyopita, Shirika la Waandishi Wasiokuwa na Mipaka (RSF) lilisema vikosi vya jeshi la Israel vimefanya "mauaji" ya waandishi wa habari wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, na kuua idadi kubwa ya wanahabari.

Vilevile Shirikisho la Kimataifa la Wanahabari (IFJ) limetangaza kuwa 2024 umekuwa mwaka wa "mauti zaidi" kwa waandishi wa habari kutokana na waandishi 104 wa habari kuuawa duniani kote, huku zaidi ya nusu kati yao wakiuawa katika Ukanda wa Ghaza.