Israel yashambulia magari 40 ya wagonjwa Ukanda wa Ghaza
Taasisi ya Ulinzi wa Raia ya Ghaza imetangaza kuwa jeshi la Israel limeshambulia na kuharibu magari 40 ya kubebea wagonjwa katika ukanda huo tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha mashambulizi yake ya kikatili yanayoendelea hadi hivi sasa dhidi ya Wapalestina.
Mahmoud Basal, Msemaji wa Taasisi ya Kulinda Wananchi ya Ghaza amesema hayo katika katika mahojiano na televisheni ya Al-Masirah wa Yemen jana jioni na kusisitiza kwamba zaidi ya Wapalestina 40 waliuawa shahidi jana pekee katika mashambulizi ya adui Mzayuni.
Ameongeza kwa kusema kuwa, Israel imewalazimisha kuhama zaidi ya Wapalestina 160,000 kutoka Ukanda wa Ghaza na imeharibu magari 40 ya wagonjwa kati ya 70 yaliyokuwepo kwenye ukanda huo.
Vilevile amesema: "Mauaji yanayofanywa na adui Mzayuni katika Ukanda wa Ghaza hayajatokea mfano wake katika karne yote ya 21."
Ukanda wa Ghaza umekuwa chini ya mashambulio ya kikatili ya utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa na kila kitu kimeharibiwa katika eneo hilo.
Wakati watu wa Ghaza wakihitajia mno chakula na madawa, Israel inaruhusu kiasi kidogo sana cha misaada ya kibinadamu kuingia Ghaza na tena baada ya kufanyiwa ukaguzi mkali.
Wizara ya Afya ya Ghaza imetangaza kuwa jeshi la Israel limeshaua shahidi Wapalestina wapatao 45,000 katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo.