Netanyahu aburuzwa tena mahakamani leo Jumatatu
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i120220-netanyahu_aburuzwa_tena_mahakamani_leo_jumatatu
Duru mbalimbali za habari zikiwemo za Kizayuni zimeripoti kwamba, waziri mkuu wa Israel ambaye ni maarufu kwa jina la nduli wa Ghaza, ameburuzwa tena mahakamani leo Jumatatu kujibu shutuma za ufisadi na jinai zinazomuandamana yeye na familia yake.
(last modified 2024-12-16T07:51:47+00:00 )
Dec 16, 2024 07:51 UTC
  • Netanyahu aburuzwa tena mahakamani leo Jumatatu

Duru mbalimbali za habari zikiwemo za Kizayuni zimeripoti kwamba, waziri mkuu wa Israel ambaye ni maarufu kwa jina la nduli wa Ghaza, ameburuzwa tena mahakamani leo Jumatatu kujibu shutuma za ufisadi na jinai zinazomuandamana yeye na familia yake.

Televisheni ya Israel imetangaza kuwa Netanyahu amefikishwa mahakamani leo saa nne asubuhi kutoa ushahidi katika kesi yake ya jinai. Kesi hiyo ilipangwa kuendelea hadi saa 10 jioni.

Kuburuzwa Netanyahu mahakamani ni sehemu ya mchakato wa kufuatiliwa mashtaka ya ufisadi, kupokea rushwa, utapeli na kukosa uaminifu.

Kesi mbili za mahakama zimefanyika dhidi ya Netanyahu katika siku za hivi karibuni.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliburuzwa mahakamani kwa mara ya kwanza tarehe 10 Disemba 2024 katika kesi yake ya ufisadi. Netanyahu amejaribu mara kwa mara kuchelewesha kusikilizwa kesi zake kwa kisingizio cha vita vinavyoendelea Gahza na masuala mengine ya kiusalama. Hata hivyo, majaji waliamuru kesi irejee lakini wameihamishia kwenye mahandaki ya chini ya ardhi katika mahakama ya Tel Aviv kwa sababu za usalama.

Netanyahu ni waziri mkuu wa kwanza wa Israel kuburuzwa mahakamani akiwa madarakani. Yeye na familia yake wana kesi za kujibu katika mashtaka ya ulaghai, kupokea rushwa, kula hongo na kukosa uaminifu.