Wakurdi wa Syria wana wasiwasi wa kutokea Syria yaliyotokea Libya
Msemaji wa kundi la SDF ambalo ni la Wakurdi wa Syria wanaoungwa mkono na Marekani amesema kuwa, wana wasiwasi wa kugeuka Syria kuwa Libya ya pili baada ya kuangushwa utawala wa Bashar al Assad.
Abdul Salam Ahmed, msemaji wa kundi linalojiita Kikosi cha Demokrasia cha Syria (SDF) kinachoungwa mkono na Marekani, amesema kuwa, Wakurdi wana wasiwasi kuhusu mustakbali wa Syria na hatari ya kushuhudiwa nchini humo hali ile ile iliyotokea Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi.
Ameongeza kuwa, kundi lao ambalo ni sehemu ya wapinzani wanaobeba silaha, lina maoni tofauti kuhusu Syria ikilinganishwa na makundi mengine yaliyoshiriki kuipindua serikali ya Bashar al Assad. Amesema, kuna hatari tutarudia hali ya Libya.
Wataalamu wanaamini kwamba kuanguka serikali ya Rais Bashar al Assad huko Syria kwa Damascus kunaweza kuwa mwanzo wa mgogoro mpya na mbaya sana nchini humo na kuna hatari pia ya kutokea machafuko kama yaliyotokea nchini Libya baada ya kupinduliwa utawala wa Muammar Gaddafi.
Tangu kuanguka Muammar Gaddafi mwezi Oktoba 2011 hadi hivi sasa, Libya imeendelea kuwa ndani ya machafuko na ukosefu wa utulivu huku sehemu kubwa za nchi hiyo ikidhibitiwa na wanamgambo.
Hivi sasa kuna serikali mbili hasimu zinatawala ndani ya nchi moja ya Libya, moja upande wa magharibi na nyingine upande wa mashariki na hakuna dalili za kutatuliwa kikamilifu mgogoro wa miaka mingi wa nchi hiyo.
Msemaji huyo wa kundi la SDF la Wakurdi wa Syria walioko chini ya jeshi vamizi la Marekani ameliambia shirika la habari la Sputnik kwamba inabidi wafuasi wa kundi hilo waungwe mkono kimataifa hasa kwa kuzingatia kuongezeka makundi ya kigaidi, kaskazini mashariki mwa Syria.