D8, nembo ya nguvu ya Ulimwengu wa Kiislamu
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, yuko Misri anakoshiriki mkutano wa 11 wa viongozi wa nchi za kundi la D8.
Akiwa Cairo, Rais Pezeshkian atahutubia mkutano wa viongozi wa D8, mkutano maalumu wa Gaza na Lebanon, na kufanya mazungumzo ya pande mbili na viongozi na wakuu wa nchi nyingine, akiwemo Rais wa Misri, Abdel Fattah al Sisi.
Mkutano wa 11 wa kilele wa nchi nane zinazoendelea za Kiislamu, kwa kifupi D8, unafanyika leo Alkhamisi mjini Cairo, ili kujadili njia za kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kisiasa katika Ulimwengu wa Kiislamu.
D8 iliundwa mwaka wa 1997 katika kikao cha viongozi wa nchi nane zinazoendelea za Kiislamu, ambazo ni Iran, Uturuki, Misri, Bangladesh, Nigeria, Indonesia, Malaysia na Pakistani, na kuzidisha matumaini ya kusaidia ustawi wa uchumi wa nchi nyingine za Kiislamu.
Safari ya Rais Pezeshkian mjini Cairo ni muhimu sana katika ngazi ya milinganyo ya kikanda na kimataifa, ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi wa nchi za Kiislamu wanachama wa D8, na pia kuandaa mipango bora zaidi ya kuanzishwa uhusiano kati ya Iran na Misri.
Kabla ya kuondoka Tehran akielekea Cairo, Rais Pezeshkian alisema: "Mikutano inayofanyika katika ngazi hii na kwa mwenendo huu wa kuwa na diplomasia amilifu ambayo inaweza kuzileta pamoja nchi za Kiislamu ili ziwe na uhusiano wa karibu zaidi wa kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii, ina taathira na faida kubwa katika mawasiliano tunayojenga katika kanda hii na kubadilishana uzoefu."
Amesema 'kadiri tutavyoweza kuboresha uhusiano wetu na nchi za Kiislamu ndivyo tutakavyoweza zaidi kuzima njama za maadui dhidi ya nchi yetu na nchi nyingine za Kiislamu".
Ameitaja Misri, mwenyeji wa mkutano huo, kuwa ni nchi yenye historia ndefu na ustaarabu mkubwa na kusema: "Misri ni nchi yenye taathira katika Ulimwengu wa Kiislamu, na pambizoni mwa mkutano wa kilele wa BRICS uliofanyika Kazan, Russia mwezi Novemba, tulikuwa na mazungumzo chanya na Rais wa Misri."
Ukweli ni kwamba Iran na Misri ni nchi mbili zenye ustaarabu wa kale na masuala ya kihistoria yanayozikutanisha pamoja; na zinaweza kuboresha nafasi yao katika milinganyo ya kieneo na kimataifa kwa kuimarisha uhusiano wa pande mbili. Kwa upande mwingine, nafasi ya kistratijia ya nchi hizi mbili inawezesha kushirikiana katika maeneo kama vile usafiri wa baharini, nishati, utalii na biashara.
Kwa msingi huo, Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Badr Abdul Ati, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Misri wamekutana pembezoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Nje wa D8 na kueleza matumaini yao kwamba mkutano huo utapata matokeo mazuri kwa kuzingatia maslahi ya mataifa ya kundi la nchi zinazostawi za Kiislamu na Ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla. Mojawapo ya masharti ya kufikiwa lengo hili ni kuimarisha zaidi mchango na nafasi muhimu na athirifu ya Iran na Misri katika kanda na Ulimwengu wa Kiislamu.
Wakati huo huo, inapaswa kuzingatiwa kuwa kuongeza ushirikiano wa kiuchumi na kuimarisha mabadilishano ya kibiashara kati ya nchi wanachama wa D8 kunaweza kuchangia kwa ufanisi mkubwa mzunguko wa kifedha na kibiashara wa kundi la nchi za Kiislamu.
Jamii ya nchi nane za G8 ni takriban watu bilioni 1.2, au 60% ya jumla ya idadi ya Waislamu, ambayo ni karibu 13% ya jumla ya idadi ya watu duniani. Nchi nane wanachama zinachukua eneo la kilomita za mraba milioni 7.6 au 5% ya eneo lote la dunia. Biashara kati ya nchi wanachama wa kundi hili ni takriban dola bilioni mia moja kwa mwaka. Mchakato wa kustawisha ushirikiano baina ya nchi wanachama wa G8 pia unatoa fursa ya kipekee ya kuwa na ufanisi katika masuala ya kisiasa na kiusalama yanayohusiana na Waislamu na kutoruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel na waungaji mkono wake kufanya jinai katika Ulimwengu wa Kiislamu, ikiwa ni pamoja na huko Gaza, Lebanon, Yemen na Syria.