Mahakama yaakhirisha kesi ya Sheikh Issa Qassim
Utawala wa Aal Khalifa leo umesikiliza kikao cha kwanza cha kesi iinayomkabili Sheikh Issa Qassim kiongozi wa Washia wa Bahrain.
Habari zinasema kuwa mahakama ya Bahrain leo asubuhi ilisikiliza kikao cha kwanza cha kesi inayomkabili Sheikh Issa Qassim Kiongozi wa Washia wa Bahrain bila ya kuwepo mwanazuoni huyo, hata hivyo mahakama hiyo imeakhirisha kesi hiyo hadi tarehe 14 Agosti.
Ahmad al Dosari Mwendesha Mashtaka wa Bahrain amedai kuwa Sheikh Qassim anatuhumiwa kwa kosa la kukusanya fedha bila ya kibali, hata hivyo Abdalllah al Shamalawi wakili anayemtetea Sheikh Issa Qassim ambaye pia ni mtetezi wa haki za binadamu amesema kuwa tuhuma zinazomkabili mwanazuoni huyo mtajika wa Bahrain ni kinyume na kipengee cha 22 cha katiba ya nchi hiyo.
Wananchi wa Bahrain jana usiku walimiminika katika mitaa mbalimbali nchini wakilalamikia kushtakiwa Sheikh Issa Qassim' ambapo walipiga nara dhidi ya hatua za kidhalimu na kiukandamizaji za utawala wa Aal Khalifa.
Wakati huo huo katika hatua yake inayokinzana na sheria za haki za binadamu, utawala wa Aal Khalifa hivi karibuni ulimfutia uraia Sheikh Issa Qassim, hatua iliyoshadidisha mivutano na malalamiko ya wananchi wa Bahrain.