Mashinikizo kwa serikali ya Iraq ya kuvunja Hashd al-Shaabi
(last modified Tue, 07 Jan 2025 10:50:46 GMT )
Jan 07, 2025 10:50 UTC
  • Mashinikizo kwa serikali ya Iraq ya kuvunja Hashd al-Shaabi

Mashinikizo ya kigeni hususan kutoka Marekani yameongezeka kwa serikali ya Iraq ili kuivunja Harakati ya Wananchi ya Hashd al-Shaabi.

Mashinikizo hayo ni makubwa kiasi kwamba, yameibana serikali ya Mohammad Shia al-Sudani Waziri Mkuu wa Iraq.

Hashd al-Shaabi ni moja ya makundi muhimu ambayo ni mwanachama wa mhimili wa muqawama, ambao umekuwa na nafasi kubwa katika mapambano ya Iraq dhidi ya ugaidi wa Daesh na umewaunga mkono watu wa Gaza katika kipindi cha miezi 15 ya kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Takwa la kuvunjwa kwa Hashd al-Shaabi lilitolewa baada ya kuanguka serikali ya Bashar Assad nchini Syria na kugeuka hatua kwa hatua kuwa shinikizo la kisiasa dhidi ya serikali ya Baghdad. Kwa hakika, kupinduliwa kwa gharama nafuu na haraka kwa serikali ya Bashar al-Assad kumeandaa uwanja wa takwa na mashinikizo hayo, kwa sababu Marekani na utawala wa Kizayuni zilifikia hitimisho kwamba muqawama umedhoofika na kuna uwezekano wa kuifuta Hashd. al-Shaabi kama moja ya nguzo muhimu zaidi za muqawama.

Mashinikizo haya yanakuja wakati ambapo Hashd al-Shaabi ilifuata mkondo wa sera iliyofungamana na serikali ya Baghdad wakati wa kupinduliwa serikali ya Bashar al-Assad, ambapo sambamba na kusimamisha mashambulizi dhidi ya utawala wa Kizayuni, ilijizuia kuingilia kati mgogoro wa Syria.

Hashd al-Shaabi iliundwa mwaka 2014 kwa fat’wa ya Kiongozi wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali al-Sistani

 

Suala jengine ni kuwa, mashinikizo ya kutaka kuvunjwa Hashd al-Shaabi yanatolewa katika hali ambayo, mwaka 2016 Harakati ya Hashd Al-Shaabi ilijumuishwa rasmi katika jeshi la Iraq na vikosi vyake vinahesabiwa kuwa sehemu rasmi ya jeshi la nchi hiyo. Ukweli wa mambo ni kuwa, lengo kuu la kuongeza mashinikizo kwa serikali ya Iraq ili kuivunja Hashd al-Shaabi ni kupunguza uwezo wa jeshi la Iraq.

Kupungua kwa vikosi vya wananchi kutasababisha jeshi kuwa dhaifu kiutendaji. Hili lilikuwa kosa ambalo serikali ya Bashar al-Assad pia ilifanya na kwa kusambaratisha vikosi vya wananchi, kivitendo ikawa imesambaratisha nguvu muhimu ya kiulinzi na kijeshi, na ikawa sababu muhimu ya kuanguka kwa kasi na kwa haraka serikali ya Bashar al-Assad.

Kwa kuzingatia kwamba Hashd al-Shaabi ni kikosi rasmi cha kijeshi cha Iraq, kuvunjwa kwake lazima kuambatane na idhini ya bunge, kwani serikali pekee haiwezi kuamua juu ya suala hili.

Ghani al-Ghadhban, mtaalamu wa masuala ya kisiasa na kiusalama ya Iraq amesema katika muktadha huo: “Serikali ya Iraq haiwezi kuvifuta kabisa vikosi vya Hashd al-Shaabi, kwa sababu uundaji wake uliidhinishwa na wabunge walio wengi, na uamuzi wowote wa kukivunja unahitaji idhini ya Bunge."

Wapiganaji wa Hashd al-Shaabi

 

Nukta nyingine muhimu ni kwamba, Hashd al-Shaabi iliundwa mwaka 2014 kwa fat’wa ya Kiongozi wa juu wa kidini na Marjaa-Taqlidi wa Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Iraq Ayatullah Sayyid Ali al-Sistani na ilikuwa ni baada ya uvamizi wa kundi la kigaidi la Daesh nchini Iraq. Kwa hiyo, walijaribu kupata ridhaa ya Ayatullah Sistani ya kuivunja harakati hii, jaribio ambalo nalo halijafanikiwa.

Mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Iraq alikutana na Ayatullah Sistani kuhusiana na kuvunjwa  Hashd al-Shaabi, lakini ombi hilo lilikabiliwa na upinzani mkali wa Marjaa huyo wa kidini wa Iraq. Kwa hiyo, tofauti muhimu kati ya Hashd al-Shaabi huko Iraq na vikosi vya wananchi nchini Syria ni kwamba, Hashd al-Shaabi ina himaya na uungaji mkono kamili wa uongozi wa kidini nchini Iraq.