Hamas kwa Waislamu kote duniani: Pingeni njama zote za Wazayuni
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imetoa wito kwa jamii ya Waislamu duniani kote, ikiwemo ile ya Palestina, kupinga njama zote za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Umma wa Kiislamu.
Hamas imesema hayo katika taarifa yake ya kuadhimisha kumbukumbu ya kuteuliwa Mtume Muhammad (saw) kuwa mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu inayosadifiana na tarehe 27 Rajab.
Kwa mujibu wa Hamas, tukio hilo la kubaathiwa Mtume linapaswa kutumika kama "wito wa kupinga njama zote za Wazayuni zinazolenga Umma wa Kiislamu na kuunga mkono kusimama thabiti kwa Wapalestina katika mji mtakatifu wa Quds unaokaliwa kwa mabavu, ambao wanaupigania kama mji mkuu wa nchi yao.
Hafla hiyo pia inataka kuwapongeza "wale wanaoendelea kusimama imara kwenye Msikiti wa al-Aqsa kwa njia zote," ikiwa ni ishara kwa wale wanaokaidi vikwazo vya utawala wa Israel dhidi ya Swala ya Waislamu katika msikiti huo, ambao unatambuliwa kama mojawapo na maeneo matakatifu kwa Waislamu duniani.
Hamas pia imesisitiza kwamba "uvamizi wa kifashisti wa Israel utashindwa kufuta utambulisho wa Kiarabu na Kiislamu wa al-Quds na al-Aqsa au kubadilisha ukweli wa kihistoria" kuhusu maeneo hayo mawili.