Ni maelfu mangapi ya mabomu ya Marekani yamewaangukia watu wa Gaza?
Taasisi moja ya Marekani imekiri kwamba Washington iliipatia Israel maelfu ya mabomu ya kuvunja mahandaki aina ya MK-84 wakati wa vita mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel dhidi ya raia wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Taasisi ya The Boston American Institute imetangaza katika ripoti yake kwamba Marekani, pamoja na kuipatia Israel mabomu 14,100 ya kuvunja mahandaki ya MK-84 kwa ajili ya mauaji ya watu wasio na ulinzi huko Gaza, pia ilitoa makombora 57,000 ya 155 mm, bunduki 20,000 za M4A1, na makombora elfu 13,981 ya kutungua ndege kwa utawala wa Kizayuni.
Rais wa Marekani, Donald Trump, pia hivi karibuni aliafiki kutuma mabomu 1,800 ambayo kila moja lina uzito wa pauni 2,000 kwa Israel. Shehena ya mabomu hayo ilisitishwa na utawala wa Joe Biden kutokana na malalamiko ya kimataifa.
Katika upande mwingine, tovuti ya Axios imewanukuu maafisa watatu wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakisema kwamba Ikulu ya White House imeliamuru jeshi la Marekani kuondoa mipaka iliyokuwa imewekwa na utawala wa Joe Biden ya kubana utoaji wa mabomu mazito kwa Israel.
Utawala wa Biden uliweka mipaka katika utoaji wa mabomu mazito kwa utawala katili wa Israel baada ya kushadidi malalamiko ya kimataifa ya kupinga mauaji ya kimbari ya utawala huo katili dhidi ya raia wa Palestina.
Karibu raia elfu khamsini wa Palestina wameuawa katika kampeni ya mauaji ya kimbari ya Israel ikisaidiwa na Marekani katika eneo la Ukanda wa Gaza.
Kufuatia mauaji hayo, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa kibali cha kukatwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita na jinai dhidi ya binadamu.