Hamas yawaachia huru mateka 3 wa Israel, mkabala wa Wapalestina 183
Utawala wa Kizayuni wa Israel baadaye leo unatazamiwa kuwaachia huru mateka 183 wa Kipalestina, mkabala wa kuachiliwa Wazayuni watatu, katika awamu ya nne ya mabadilishano ya mateka katika Ukanda wa Gaza.
Televisheni ya al-Jazeera ya Qatar imeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Hamas imewataja Waisraeli watatu walioachiliwa huru leo kuwa ni Ofer Kalderon, Keith Siegel na Yarden Bibas. Hadi tunaingia mitamboni, mateka wawili kati ya watatu hao tayari walikuwa wamekwishaachiwa huru.
Habari zaidi zinasema kuwa, baada ya Hamas kuwasilisha orodha ya mateka watakaoachiliwa huru leo Jumamosi, Israel nayo imetangaza kuwa itawaachia huru wafungwa 183 wa Kipalestina.
Haya yanajiri siku mbili baada ya utawala wa Kizayuni kuwaachilia huru mateka 110 wa Kipalestina mkabala wa kuachiliwa Wazayuni watatu na raia watano wa Thailand.
Aidha Januari 26, Wapalestina 200 waliokuwa wakishikiliwa katika magereza ya utawala haramu wa Israel waliachiliwa huru ikiwa ni sehemu ya makubaliano ya ubadilishanaji mateka baina ya Israel na Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas.

Chini ya makubaliano hayo ya kusitishwa kwa mapigano na kubadilishana mateka, bidhaa muhimu kama vile, mafuta, chakula na misaada ya matibabu imeanza kuwasilishwa katika Ukanda wa Gaza.
Tel Aviv ilisalimu amri na kukubali kusani kuakubaliano ya kusitisha mapigano na vita vya kinyama na mauaji ya kimbari yaliyofanywa na utawala huo wa Kizayuni kwa siku 471 katika Ukanda wa Gaza, ambapo Wapalestina 47,460 waliuawa shahidi.