Hamas: Witkoff aliahidi kuondoa mzingiro wa Gaza mkabala wa kuachiwa Edan Alexander
(last modified Sat, 17 May 2025 10:27:24 GMT )
May 17, 2025 10:27 UTC
  • Hamas: Witkoff aliahidi kuondoa mzingiro wa Gaza mkabala wa kuachiwa Edan Alexander

Afisa mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas amesema kuwa, mjumbe maalumu wa Marekani Steve Witkoff alilihakikishia kundi hilo la Muqawama la Palestina kwamba, Washington itaishinikiza Israel kukomesha mzingiro wa Gaza na kuruhusu ufikishaji wa misaada ya kibinadamu ndani ya siku mbili baada ya kumwachilia huru mwanajeshi wa Israel, Edan Alexander, raia wa Marekani.

Basem Naim, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas ambaye hapo awali alifanya mazungumzo ya moja kwa moja na maafisa wa Marekani, aliiambia 'Drop Site' kuwa, Witkoff pia aliahidi kwamba, Trump atatoa mwito hadharani wa kusitishwa mara moja kwa mapigano huko Gaza na kufanyika mazungumzo yenye lengo la kufikia "usitishwaji wa kudumu wa vita."

"Haya ndiyo yalikuwa makubaliano," Naim amesisitiza na kuongeza kwamba, "Ahadi hiyo ilitolewa na Witkoff mwenyewe." Akizungumzia mpango huo, afisa huyo wa Hamas amesema, "Ikiwa tutamwachilia [Alexander], Trump atazungumza akiishukuru Hamas kwa nia yake, na kuilazimisha Israel katika siku ya pili kufungua mipaka na kuruhusu misaada kuingia Gaza, na [Trump] angelitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja na kuingia kwenye mazungumzo ya kumaliza vita."

Kuwa mujibu wa Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, "(Witkoff) Hakufanya chochote kuhusiana na hili. Hawakukiuka mpango huo (tu, bali) waliutupa kwenye jaa la taka." Wiki hii wakiwa mjini Doha, Qatar, Witkoff na Adam Boehler, Mjumbe Maalumu wa Ikulu ya White House kuhusu wafungwa, walifanya mazungumzi ya kina na wapatanishi wa Israel na wa kikanda kutoka Qatar na Misri.

Ingawaje maafisa wote wa Marekani walionyesha matumaini kuhusu mafanikio yanayoweza kufikiwa, lakini Basem Naim, Mjumbe wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas alipuuzilia mbali uwezekano wowote wa kupigwa hatua. "Sifuri, sifuri kubwa," alisema Naim.

Ikumbukwe kuwa, Hamas ilisema imekubali kumwachilia huru Muisraeli Mmarekani, Edan Alexander aliyekuwa anashikiliwa huko Gaza, baada ya kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Marekani kuhusu kusitishwa mapigano katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa kila upande na Wazayuni.