"Kuuawa viongozi wa Muqawama kunaimarisha irada ya Wapalestina"
(last modified Mon, 09 Jun 2025 02:49:04 GMT )
Jun 09, 2025 02:49 UTC

Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina imelaani vikali mauaji ya Israel dhidi ya afisa mashuhuri wa Muqawama na watu wengine 30 katika mji wa Gaza na kusisitiza kuwa, mauaji hayo yanayolenga viongozi wa mrengo wa mapambano kamwe hayatadhoofisha uthabiti na azma ya wananchi wa Palestina.

Katika taarifa yake iliyotolewa jana Jumapili, harakati hiyo yenye makao yake Gaza imesema kuwa, kuuawa shahidi Sheikh Asaad Abu Sharia, Katibu Mkuu wa Harakati ya Mujahidina, sawa na makamanda wengine wakuu wa Muqawama, kutaimarisha azma na irada ya Wapalestina wa matabaka yote. Imebainisha kuwa, jinai hizo zitawatia moyo na kuwashajiisha Wapalestina kuendelea na njia ya mapambano na kukabiliana na adui Mzayuni kwa uthabiti zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa, kiongozi huyo wa Harakati ya Mujahidina ya Palestina aliyeuawa na kaka yake Ahmed Abu Sharia, walitembelea njia ndefu ya jihadi, uthabiti na kujitolea muhanga kupambana na utawala wa Kizayuni, na walikuwa waaminifu na waungaji mkono wakubwa wa taifa lao. "Tunasisitiza kwamba, kulengwa makamanda na utawala wa kihalifu (wa Israel) kutaimarisha tu azma ya taifa letu ya kuendeleza njia ya Muqawama na kulinda ardhi yetu," Harakati ya Jihadul Islami imesema.

Haya yanajiri siku moja baada ya Abu Ubaida, Msemaji wa Brigedi za al-Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina Hamas kusisitiza kwamba, operesheni za wanamuqawama dhidi ya uvamizi wa Israel zitaendelea "hadi pale utawala wa Kizayuni utakaposhindwa." Makundi ya Muqawama ya Wapalestina yalifanya msururu wa operesheni zenye mafanikio katika eneo la Khan Yunis siku ya Ijumaa, zikilenga maeneo muhimu ya kijeshi ya Israel, wakati ambapo utawala wa Kizayuni unapoendeleza mashambulizi ya kinyama katika Ukanda wa Gaza.