Israel yaua mwandishi mwingine wa Kipalestina, idadi ya waliouawa yafika 229
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i128182
Ofisi ya serikali ya vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa mwandishi habari mwingine wa Kipalestina ameuawa katika shambulio la Israel katika eneo hilo lililozingirwa kinyume cha sheria, na kuongeza idadi ya wanahabari waliouawa imefika 229 tangu Oktoba 2023, wakati utawala dhalimu wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Gaza.
(last modified 2025-07-11T08:54:38+00:00 )
Jul 11, 2025 07:40 UTC
  • Ahmad Abu Aisha
    Ahmad Abu Aisha

Ofisi ya serikali ya vyombo vya habari katika Ukanda wa Gaza imetangaza kuwa mwandishi habari mwingine wa Kipalestina ameuawa katika shambulio la Israel katika eneo hilo lililozingirwa kinyume cha sheria, na kuongeza idadi ya wanahabari waliouawa imefika 229 tangu Oktoba 2023, wakati utawala dhalimu wa Israel ulipoanzisha mashambulizi ya kinyama dhidi ya Gaza.

Taarifa ya Alhamisi imesema kuwa Ahmad Abu Aisha, mwandishi wa Palestine Today TV, alipoteza maisha baada ya kupigwa moja kwa moja na kombora la droni ya Israel akiwa mbele ya nyumba yake katika eneo la Sawarha, magharibi mwa kambi ya wakimbizi ya Nuseirat katikati mwa Gaza.

Ofisi hiyo imelaani vikali “mauaji ya makusudi dhidi ya waandishi wa habari wa Kipalestina,” na kutaka taasisi za haki za binadamu na vyombo vya habari duniani “kutoa msimamo thabiti kulaani uhalifu huu unaolenga kuangamiza sauti ya haki Gaza.”

Chama cha Waandishi wa Habari wa Palestina kimelaani mauaji hayo kuwa ni jinai ya makusudi ambayo imelenga kubana sauti ya ukweli. Walisisitiza kuwa mwandishi huyo alilengwa moja kwa moja akiwa hana silaha, akitekeleza wajibu wake wa kitaaluma na wa kizalendo mbele ya nyumba yake.

Chama hicho kilikemea sera ya makusudi ya Israel ya kuwalenga waandishi na taasisi za habari, jambo linalokiuka waziwazi sheria ya kimataifa ya kibinadamu, inayolinda waandishi wa habari katika maeneo ya migogoro.

Kimeitaka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ichukue hatua ya haraka na kuwawajibisha viongozi wa Israel kwa uhalifu wao dhidi ya waandishi wa habari.

Taarifa hiyo imesema: “Waandishi wa Palestina sasa wamekuwa walengwa ,  si kwa kosa lolote, bali kwa kutimiza jukumu lao la kuueleza ulimwengu ukweli wa unyama unaoendelea Gaza.” 

Duru rasmi Palestina zimedokeza kuwa tangu Oktoba 7, 2023 hadi sasa, takriban 57,762 Wapalestina, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa, na wengine 137,656 wamejeruhiwa katika mashambulizi makali ya mauaji ya kimbari yanayoendeshwa na Israel dhidi ya Gaza, eneo linalozingirwa na kunyimwa haki za kibinadamu kwa miongo kadhaa.

Mwezi Novemba mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) ilitoa hati za kukamatwa kwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na aliyekuwa Waziri wavita Yoav Gallant, kwa mashitaka ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Zaidi ya hayo, Israel inakabiliwa na kesi ya mauaji ya kimbari (genocide) katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na vita vyake vya kikatili dhidi ya taifa la Palestina, hususan Gaza.