Kwa nini maelfu ya Wazayuni wanataka kusimamishwa vita vya Gaza?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130648-kwa_nini_maelfu_ya_wazayuni_wanataka_kusimamishwa_vita_vya_gaza
Maelfu ya Wazayuni wamefanya maandamano ya kumpinga Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na kutaka kusitishwa mara moja vita vya Ukanda wa Gaza na kukombolewa mateka wa Kizayuni.
(last modified 2025-09-10T13:37:52+00:00 )
Sep 10, 2025 13:37 UTC
  • Kwa nini maelfu ya Wazayuni wanataka kusimamishwa vita vya Gaza?

Maelfu ya Wazayuni wamefanya maandamano ya kumpinga Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni na kutaka kusitishwa mara moja vita vya Ukanda wa Gaza na kukombolewa mateka wa Kizayuni.

Maelfu ya Wazayuni walimiminika katika mitaa ya Tel Aviv Jumamosi ya tarehe 6 Septemba wakiwataka watawala wa utawala wa Kizayuni wasimamishe vita vya Gaza mara moja na kufanya juhudi za kuachiliwa huru mateka wa Kizayuni huko Gaza. Waandamanaji pia walipinga mipango ya Netanyahu ya kukalia kwa mabavu mji wa Gaza.

Waandamanaji hao wa Kizayuni wanaamini kuwa operesheni hiyo inaweza kuhatarisha maisha ya mateka waliosalia Gaza. Kadhalika, baadhi ya vyombo vya habari katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu vimeripoti kuwa, mamia ya Wazayuni walifanya maandamano mbele ya nyumba ya Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni huko Beitul Muqaddas inayokaliwa kwa mabavu.

Maandamano hayo ya wakaazi wa maeneo yanayokaliwa kwa mabavu dhidi ya Netanyahu na sera zake za kivita yaligeuka kuwa ghasia na makabiliano na vikosi vya polisi dhidi ya waandamanaji. Vyombo vya habari vya Kizayuni vimeripoti kuwa polisi wa utawala wa Kizayuni waliwatia mbaroni waandamanaji kadhaa wanaopinga vita katika maandamano hayo.

Wazayuni wapambana na polisi 

Kufuatia uamuzi wa Netanyahu na baraza la mawaziri la utawala wa Kizayuni wa kuikalia kikamilifu Gaza, wimbi kubwa la maandamano na hasira za Wazayuni limeongezeka ambapo waandamanaji wamekuwa wakifanya maandamano kila wiki kupinga siasa za Netanyahu. Wazayuni wengi wanataka kuhitimishwa vita hivyo wanapinga vikali uamuzi wa waziri mkuu huyo mtenda jinai wa kuendelea kupanua vita.

Maandamano yaliyoenea katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu ya kupinga vita vya Gaza na kukaliwa kwa mabavu kikamilifu ukanda huo si tu ni ishara ya mgawanyiko mkubwa ndani ya utawala wa Kizayuni, bali pia ni dhihirisho la mgogoro wa uhalali wa kisiasa na kimaadili wa utawala huo katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na katika maeneo mengine ya dunia.

Familia za mateka wa Kizayuni zinaamini kuwa, serikali ya Netanyahu inaendeleza vita kwa sababu za kisiasa na ndio maana inazuia kuachiliwa kwao. Kwa upande mwingine, Netanyahu anategemea uungaji mkono wa Wazayuni wenye misimamo mikali ya kufurutu ada ili kudumisha utawala wake, ambao wanapinga juhudi zozote za kusitisha vita.

Vizuizi katika barabara kuu, matairi yanayowaka moto, na mikutano ya hadhara mjini Tel Aviv, yote hayo yanaonyesha hasira ya umma na kupungua imani kwa serikali. Maoni ya jamii ya kimataifa pia yanapinga siasa za jinai za utawala wa Kizayuni. Tangu kuanza kwa vita vya Gaza, mamilioni ya watu duniani kote wamejitokeza kupinga hatua za mauaji ya umati za utawala wa Israel. Maandamano yameenea sio tu katika nchi za Kiislamu bali hata Ulaya, Marekani na Asia.

Utumiaji wa silaha za maangamizi ya halaiki na jeshi la utawala wa Kizayuni ikiwemo fosforasi nyeupe, mashambulizi katika maeneo salama na kulazimishwa Wapalestina kuyahama makaazi yao kumepelekea ibara kama mauaji ya halaiki na ukaliaji mabavu zitumike mara kwa mara katika mikutano ya hadhara na vyombo vya habari.

Baraza la mawaziri la Netanyahu linakabiliwa na mashinikizo ya ndani na nje ambapo maamuzi yake yanakosolewa vikali na wapigania amani kote ulimwenguni. Majeruhi wengi raia, hali mbaya ya kibinadamu huko Gaza na picha za kutisha za mauaji ya kizazi pia zimeamsha hasira ya umma kimataifa na hivyo kuibua maandamano makubwa kimataifa.

Hali ya Tel Aviv pia si nzuri kwa Netanyahu, ambapo vyama vya upinzani vinamtuhumu kwa kusema uwongo kuhusu vita vya Gaza na kushindwa kuvidhibiti. Baadhi ya wajumbe wa Baraza la Mawaziri wanaunga mkono kwa dhati kuendelezwa vita na kukaliwa Gaza kikamilifu pamoja na kufutwa kabisa Hamas, katika hali ambayo makamanda wa utawala wa Kizayuni wamekuwa wakionya mara kwa mara kwamba jeshi la utawala huo halina uwezo wa kukabiliana na makundi ya muqawama ya Palestina hasa Hamas.

Hitilafu kali kati ya mirengo yenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia na Wazayuni wachochezi wa vita zinaweza kusambaratisha baraza la mawaziri kutoka ndani na hivyo kuutumbukiza utawala wa Kizayuni katika kipindi kirefu cha machafuko ya kisiasa. Maandamano ya Tel Aviv na maeneo mengine yanayokaliwa kwa mabavu si tu kwamba ni matokeo ya vita vya Gaza, bali pia ni taswira ya mgogoro mkubwa zaidi wa muundo wa kisiasa na kijamii katika maeneo hayo yanayokaliwa kwa mabavu. Kuendelea kwa hali hii bila shaka kutapelekea kuongezeka kwa mgogoro wa ndani na hivyo kuongeza kasi ya kusambaratika kisiasa utawala huo.