'Hatuogopi kuuawa shahidi': Mkuu mpya wa Hamas atoa ujumbe wa kwanza
-
Khalil al- Hayya, Mkuu mpya wa Idara ya Kisiasa ya Hamas
Khalil al-Hayya, mkuu mpya wa Idara ya Siasa ya Hamas, ametangaza katika ujumbe wake wa kwanza kama kiongozi wa harakati hiyo kwamba muqawama wa Palestina hautatishwa na mauaji ya wanawe au mauaji ya makamanda wake.
"Tunawaambia wavamizi kwamba sisi ndio wamiliki wa Palestina. Kuuawa kwa watoto wetu wala kuuawa viongozi wetu hakutatutisha au kututia hofu," amesema al Hayya.
Kiongozi huyo mkongwe wa Hamas alichaguliwa Jumatatu hii, akichukua nafasi iliyoachwa wazi na Yahya Sinwar, ambaye aliuawa shahidi na wanajeshi wa Israel huko Gaza mnamo Oktoba 2024.
Al Hayya, mshirika wa karibu wa Sinwar, alikuwa mjumbe mkuu wa Hamas wakati wa mazungumzo ya kusitisha mapigano na alionekana kama mtu muhimu katika harakati hiyo baada ya kuuawa shahidi Sinwar na Ismail Haniyeh.
Khalil al-Hayya ambaye alizaliwa mwaka wa 1960 katika Ukanda wa Gaza, amekuwa sehemu ya harakati ya Hamas tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 1987 na ana shahada ya uzamivu katika taaluma za Kiislamu.
Al Hayya alihudumu kama naibu wa Sinwar na alichukua uongozi wa harakati ya Hamas huko Gaza Oktoba 2024 baada ya mauaji ya Sinwar.
Amekuwa kinara wa timu ya Hamas katika mazungumzo ya kusitisha mapigano, akiongoza wajumbe katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Israel kupitia wapatanishi nchini Misri na Qatar.
Mwanamapambano huyo wa Kipalestina amenusurika majaribio mengi ya mauaji ya utawala wa kigaidi wa Israel.
Mnamo Septemba 2025, alinusurika shambulio la Israel lililolenga mkutano wa viongozi wa Hamas huko Doha nchini Qatar, na kuwaua wanachama watano wa ngazi ya chini wa kundi hilo, akiwemo mmoja wa wanawe.
Mwaka 2007, shambulio la anga la Israel kwenye nyumba ya familia yake liliwaua jamaa zake wanane. Wanawe wawili waliuawa katika mashambulizi ya awali ya Israel, na wa nne aliuawa katika shambulio la Israel huko Gaza mwezi Mei.
Mwanawe mwingine, Hamza, aliyekuwa kamanda katika kikosi cha Qassam Brigades, aliuawa katika mapigano dhidi ya wanajeshi vamizi wa Israel mwaka wa 2008.
Khalil al-Hayya anachukua hatamu za uongozi wa Hamas wakati utawala vamizi wa Isarel ukiendelea kufanya ukatili na mauaji dhidi ya watu wa Gaza, huku Hamas ikiendelea kupambana na uvamizi huo.