Aug 31, 2016 13:23 UTC
  • Watu 20 wauawa katika mashambulio ya Saudi Arabia nchini Yemen

Watu wasiopungua 20 wameuawa nchini Yemen na makumi ya wengine kujeruhiwa katika mashambulio mapya ya anga ya Saudi Arabia katika nchi hiyo.

Kanali ya Televisheni ya al-Masira imetangaza kuwa, mashambulio anga ya Saudia yaliyolenga makazi ya watu jirani na Chuo cha Kijeshi mjini Sana'a yamepelekea raia wanne kuuawa.

Taarifa ya televisheni ya al-Masira imeongeza kuwa, raia wengine 16 wameuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa katika shambulio jingine la ndege za kijeshi za Saudia katika mji wa Saida.

Wengi wa waliuawa katika shambulio la mjini Saida ni wanawake na watoto wadogo. Mashambulio hayo mapya ya Saudia yamefanyika siku moja tu baada ya Umoja wa Mataifa kuthibitisha kwamba, hujuma na mashambulio ya muungano vamizi unaoongozwa na Saudi Arabia dhidi ya nchi hiyo masikini ya Kiarabu yameua zaidi ya watu elfu kumi.

Athari ya mashambulio ya Saudia nchini Yemen

Tangu ulipoanzisha uvamizi wake wa kijeshi dhidi ya Yemen mnamo mwezi Machi mwaka uliopita, hadi sasa muungano vamizi wa kijeshi unaoongozwa na utawala wa Aal Saud na kuungwa mkono na Marekani umeshazishambulia skuli, hospitali, maeneo ya makaazi ya raia, barabara, masoko na kambi za wakimbizi na kuua maelfu ya raia wasio na hatia wa nchi hiyo.

Mashambulio hayo aidha yameharibu asilimia kubwa ya miundombinu ya nchi hiyo na kuifanya nchi hiyo iwe katika hatari ya kukabiliwa na maafa ya kibinadamu.

Tags