Rais wa Iran akosoa uungaji mkono wa US, EU kwa jinai za Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i117276
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezikosoa vikali Marekani na nchi za Ulaya kwa kuunga mkono jinai zinazofanywa na utawala khabithi wa Israel.
(last modified 2025-07-15T05:05:40+00:00 )
Oct 08, 2024 12:00 UTC
  • Rais wa Iran akosoa uungaji mkono wa US, EU kwa jinai za Israel

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amezikosoa vikali Marekani na nchi za Ulaya kwa kuunga mkono jinai zinazofanywa na utawala khabithi wa Israel.

Akizungumza leo Jumanne mjini Tehran katika hafla ya kuzindua turathi za kihistoria za zama za Hakhamaneshi (Achaemenid) zilizokuwa zimeporwa hapa Iran na kuhifadhiwa nchini Marekani kwa miongo kadhaa iliyopita, Rais Masoud Pezeshkian ameyakosoa mataifa ya Magharibi kwa kuunga mkono utawala wa Kizayuni.

Dakta Pezeshkian ameeleza bayana kuwa, "Wanashambulia wanawake, watoto, vijana, na wazee, kisha wanadai kuwa wao ni watetezi wa haki za binadamu."

Rais Pezeshkian amesisitizia umuhimu wa umoja na mshikamano kwa shabaha ya kuzuia maadui kushadidisha na migogoro na matatizo katika eneo hili.

Rais wa Iran ameongeza kuwa, kuendelea jinai za kutisha za utawala ghasibu wa Israel kunatokana na kuwepo hitilafu na mirengo kati ya mataifa ya Kiislamu; na hivyo ametoa mwito wa kuimarishwa umoja dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Maandamano ya kuadhimisha mwaka mmoja wa Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa

Mwaka mmoja baada ya kujiri Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa; utawala haramu wa Israel unaendeleza mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza. 

Zaidi ya Wapalestina 42,000 wameuawa shahidi wakiwemo 25 waliouawa usiku wa kuamkia leo katika kambi ya wakimbizi ya Bureij katikati ya Gaza. Aidha mamia ya misikiti, shule, vituo vya afya, hospitali, makazi ya raia na miundombinu imebomolewa na kuharibiwa kabisa katika kipindi cha mwaka mmoja cha mashambulio ya kinyama ya utawala ghasibu wa Israel huko Gaza.