Misri: Mgogoro wa Syria utatuliwe kupitia mazungumzo
Rais wa Misri amesema njia bora ya kutatua mgogoro wa Syria ni kupitia mazungumzo na wala sio nguvu za kijeshi.
Abdul Fattah al-Sisi amesema hayo wakati wa mkutano wake na ujumbe wa wanahabari kutoka Kuwait. Mbali na kusisitiza umuhimu wa kushadidishwa vita dhidi ya ugaidi na misimamo mikali Mashariki ya Kati na duniani kwa ujumla, kiongozi huyo amesema mgogoro wa Syria unaweza kutatuliwa kwa njia za kisiasa. Ametahadharisha juu ya njama za kuigawa Syria na kusisitiza kwamba utatuzi wowote sharti ulinde umoja wa ardhi ya nchi hiyo na uhuru wake wa kujitawala.
Rais wa Misri pia amesema lazima kuwe na mikakati ya kuijenga upya Syria baada ya miaka 5 ya mapigano. Al-Sisi amesema msimamo wa nchi yake kuhusiana na kadhia ya Syria uko wazi na kwamba Cairo itazidi kuhimiza mazungumzo kama njia pekee ya kuupatia ufumbuzi mgogoro ulioko.