Al-Sisi: Polisi wote wanakaokiuka sheria, wachukuliwe hatua kali
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1582-al_sisi_polisi_wote_wanakaokiuka_sheria_wachukuliwe_hatua_kali
Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametaka kuchukuliwa hatua kali dhidi ya polisi watakaohusishwa na ukiukaji wa sheria nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 20, 2016 04:05 UTC
  • Al-Sisi: Polisi wote wanakaokiuka sheria, wachukuliwe hatua kali

Rais Abdel Fattah el-Sisi wa Misri ametaka kuchukuliwa hatua kali dhidi ya polisi watakaohusishwa na ukiukaji wa sheria nchini humo.

Al-Sisi aliyasema hayo hapo jana ambapo alitaka pia kupandishwa kizimbani polisi wote ambao wamehusika na uvunjivu wa sheria kwa namna moja ama nyingine hususan katika kadhia nzima ya kuamiliana vibaya na watuhumiwa. Aidha akitoa pendekezo hilo kwa lengo la kukabiliana na ukiukaji wa sheria unaofanywa na polisi ya Misri, Rais al-Sisi amelitaka pia bunge kupasisha sheria kali dhidi ya polisi ambao watahusishwa na kesi hizo nchini humo. Hayo yanajiri katika hali ambayo, kwa mara kadhaa taasisi za ndani na za kimataifa kwa mara kadhaa zimekuwa zikivituhumu vyombo vya usalama nchini Misri kwa ukiukaji mkubwa wa haki za binaadamu katika kuamiliana na watuhumiwa. Kwa mujibu wa taasisi hizo, polisi ya Misri imekuwa ikitumia nguvu ya kuchupa mipaka kwa kuwapiga na kuwakandamiza wafungwa suala ambalo mara zote limekuwa likinyamaziwa na serikali ya Rais Abdel Fattah el-Sisi. Wakati huohuo tarehe 12 Februari, maelfu ya madaktari nchini Misri waliandamana hadi mbele ya makao makuu ya jumuiya ya madaktari katika mji mkuu Cairo, kulalamikia kuachiliwa huru askari polisi tisa ambao waliwapiga na kuwajeruhi madaktari wawili wa hospitali ya al-Matariyyah iliyoko mashariki mwa Cairo. Hata hivyo polisi walikabiliana vikali na madaktari hao.