Oct 28, 2016 08:03 UTC
  • Saudia yasimamisha kuwapa viza raia wa Misri

Katika hali inayoonekana ni kuongezeka mzozo baina ya Riyadh na Cairo, Saudi Arabia imechukua hatua mpya ya kushangaza ya kusimamisha kutoa viza kwa raia wa Misri.

Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na ubalozi wa Saudia huko Cairo, mji mkuu wa Misri imesema kuwa, sasa raia wa nchi hiyo hawatopewa viza za kusafiria kuelekea nchini Saudia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Shirika la Kimataifa la Tasheel ambalo lina jukumu la kutoa viza za Saudi Arabia nchini Misri, limetangaza kuwa, ubalozi wa Saudia mjini Cairo kwa sasa umesimamisha viza kwa raia wa nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Wakati watawala wa Saudia na Misri walipokuwa waitifaki wakubwa

Sambamba na Riyadh kusimamisha viza kwa raia wa Misri, mwanzoni mwa mwezi huu, Shirika la Mafuta la Saudia Aramco, lilitangaza kusimamisha kutuma mafuta ya msaada kwa Misri. Mgogoro baina ya Misri na Saudia ulishadidi baada ya serikali ya Cairo kuunga mkono muswada wa azimio la Russia mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusiana na Syria, suala ambalo liliichukiza sana Riyadh.

Watawala hao wakiwa wamekaa pamoja siku za nyuma

Hii ni katika hali ambayo utawala wa Aal Saud ulikuwa unapinga sana muswada huo wa Russia. Mbali na hilo, hatua ya Misri ya kutangaza kujiondoa katika muungano wa Saudia dhidi ya Yemen, ni suala jingine lililowakasirisha mno watawala wa kifalme wa Saudia.

Tags