Hujuma ya ndege za Marekani yaua makumi ya watu Afghanistan
Makumi ya watu wameuawa katika shambulio la anga lililofanywa na ndege za Marekani, kaskazini mwa Afghanistan.
Mahmood Danish, msemaji wa mkoa wa Kunduz, kaskazini mwa nchi hiyo amethibitisha kutokea hujuma hiyo ya kinyama na kusema kuwa, zaidi ya raia 30 wameuawa na makumi ya wengine wamejeruhiwa.
Ameongeza kuwa, aghalabu ya waliouawa katika shambulio hilo la ndege za Marekani ni wanawake na watoto wadogo na kubainisha kuwa, yumkini idadi ya waliouawa ikaongezeka kutokana na hali mbaya ya majeruhi.

Novemba mwaka jana, Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ilitangaza kuwa raia zaidi ya 40 waliuawa katika shambulio lililofanywa na ndege za kivita za Marekani dhidi ya hospitali ya jumuiya hiyo katika mji wa Kunduz nchini Afghanistan mnamo Oktoba 3 mwaka jana. Jumuiya hiyo ilisema shambulio hilo lilifanyika kwa makusudi kwa ajili ya kuua watu na kufanya uharibifu na kwamba ilikuwa ni jinai ya kivita ya wazi.
Mbali na hujuma za anga za Marekani na waitifaki wake, Afghanistan imekuwa ikishuhudia pia mashambulizi ya mabomu ya makundi ya kigaidi ya Taliban na Daesh.
Mwezi uliopita, watu 50 waliuawa na kujeruhiwa katika mripuko wa bomu uliotokea kwenye mkusanyiko wa maombolezo ya Ashura ya Imam Hussein (as) katika jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan.