Nov 14, 2016 04:06 UTC
  • Kukiri rasmi Saudia kuhusu matatizo ya kifedha yanayoiandamana

Baada ya kuenea ripoti mbalimbali za kimataifa juu ya kupungua pato la fedha linalotokanal na mafuta, hatimaye Waziri wa Fedha wa Saudia ametangaza rasmi kuwa, hivi sasa serikali ya nchi hiyo inadaiwa mamilioni ya Dola kutokana na mgogoro wa fedha.

Mohammed Al-Jadaan amesema kuwa, matatizo ya kifedha yanayotokana na kupungua kwa bei ya mafuta katika soko la dunia, yameisababishia serikali ya nchi hiyo matatizo makubwa, ikiwa ni pamoja na kudaiwa kiasi kikubwa cha mabilioni ya Dola katika sekta maalumu muhimu nchini.

Mohammed Al-Jadaan, Waziri wa Fedha wa Saudia 

Sambamba na matamshi hayo ya Mohammed Al-Jadaan, baraza la masuala ya kiuchumi na ustawi la nchi hiyo ambalo linasimamiwa na Mohammad Bin Salman, Mrithi wa Kiti cha Ufalme amesema kuwa serikali imeakhirisha mpango wa ulipaji wa madeni yake kwa sekta binafsi kutokana na kupungua kwa pato linalotokana na mauzo ya mafuta. Kwa mujibu wa ripoti ya Mfuko wa Fedha wa Kimataifa IMF, Saudia inakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti ambayo haijawahi kushuhudiwa ya karibu Dola bilioni 100 na kwamba endapo matatizo hayo hayatatatuliwa, basi muundo wa kisiasa, kiuchumi na kijamii wa nchi hiyo utakumbwa na matatizo makubwa zaidi.

Watawala wa Saudia wanaopenda vita na kuifilisi nchi huko Saudia

Kuporomoka kwa bei ya mafuta kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita ambako kulisababishwa na Saudia yenyewe, kumeulazimisha utawala Riyadh kubana matumizi ili kufidia nakisi ya bajeti. Kadhalika katika fremu hiyo serikali ya nchi hiyo imechapisha hundi za kuomba mkopo wa fedha huku ikisitisha pia uwekezaji katika sekta tofauti. Inafaa kuashiria kuwa, miaka miwili iliyopita Saudia ambayo ni mzalishaji mkubwa wa mafuta duniani iliamua kuongeza kiwango cha uzalishaji wake wa mafuta na kuyauza kwa bei ya chini sana, kwa ajili eti ya kuwaondoa washindani wake katika soko la mafuta duniani.

Moja ya ndege za Saudia zinazohusika na mauaji Yemen

Saudia baada ya kufeli siasa zake katika eneo hususan Iraq na Syria, na kwa kushirikiana na waitifaki wake ilikuwa na lengo la kutoa pigo kwa washindani wake yaani Iran, Russia na Iraq. Hata hivyo hatua hiyo ya kushusha bei ya mafuta duniani ilikuwa na matokeo kinyume na ilivyotarajia, kwani hii leo Saudia na washirika wake wa Kiarabu, wanavuna matunda ya mgogoro waliojipandikizia wenyewe. Hii ni kusema kuwa kwa mujibu wa ripoti  za asasi za kifedha duniani, nchi za Kiarabu tajiri kwa mafuta za eneo la Ghuba ya Uajemi, zinakabiliwa na nakisi kubwa ya bajeti ya kiasi cha Dola bilioni 150 kwa mwaka huu pekee. Asasi za kimataifa kama vile Mfuko wa Fedha wa Kiamataifa (IMF) na Shirika la Ustawi Duniani, sanjari na kutahadharisha juu ya hali mbaya ya kifedha ya nchi za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi hususan Saudia, zimetangaza kuwa ikiwa usimamizi mbaya wa sekta za fedha na pia mwenendo wa kukosekana uzingatiaji wa kiwango stahiki kwa ajili ya maisha ya raia wa kawaida utaendelea ndani ya mataifa hayo, basi tawala za nchi hizo zitakuwa hatarini.

Shirika la Mafuta la Saudia, ARAMCO

Katika mazingira hayo wanaharakati wa haki za binaadamu nchini Saudia na katika eneo la Mashariki ya Kati wanaamini kuwa, ufisadi na uingiliaji wa kijeshi na kisiasa wa Riyadh katika masuala ya nchi nyingine za eneo ni mambo ambayo yameathiri pakubwa uchumi wa nchi hiyo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana raia wa Saudia katika miaka ya hivi karibuni sanjari na kufanya maandamano ya kupigania haki zao za kijamii, wakataka pia kufanyike marekebisho ya kisiasa na kiuchumi nchini humo. Hata hivyo watawala wa kifalme wa nchi hiyo sanjari na kufanya mabadiliko madogo ya kimaonyesho wana lengo la kuzima kabisa malalmiko hayo ya wananchi.

 

Tags