Nov 16, 2016 02:56 UTC
  • Marekani yatuhumiwa na ICC kutenda jinai za kivita Afghanistan

Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ametoa taarifa akiituhumu Marekani kwamba, imetenda jinai za kivita nchini Afghanistan.

Fatou Bensouda amesema kuwa, baada ya kufanyika uchunguzi, nyaraka za mahakama hiyo yenye makao yake mjini The Hague Uholanzi zinaonyesha kuwa, askari wa Marekani na Shirika la Kijasusi la nchi hiyo CIA liliwatesa kinyama wafungwa baina ya mwaka 2003 na 2004. Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC amesisitia kuwa, taarifa walizonazo zinaonyesha kuwa, askari wa Marekani na maafisa wa CIA walitenda jinai kubwa wakati wa kuwasaili wafungwa.

Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC kufanya uchunguzi kuhusiana na jinai za kivita za vikosi vya Marekani nchini Afghanistan. inaonekana kuwa, hatua ya mahakama ya ICC ya kuitia hatiani Marekani ni hatua moja mbele katika njia ya kukabiliana kisheria na vitendo vya jinai vya wanajeshi na maafisa wa Shirika la Kijasusi la Marekani CIA huko nchini Afghanistan. Hadi sasa Marekani ndiyo ambayo daima imekuwa mshika bango la kutoa tuhuma dhidi ya wengine na kujionyesha kwamba, ni mtetezi wa haki za binadamu, ambapo kila mwaka hukaa na kujadili utendaji wa mataifa mengine duniani kuhusiana na suala la haki za binadamu na imekuwa ikizituhumu nchi nyingi ulimwengu kwamba, zinakiuka haki za binadamu.

Makao makuu ya ICC The Hague Uholanzi

Serikali ya Marekani daima imekuwa ikitaka kufuatiliwa na kutiwa mbaroni viongozi waliohusika na jinai za kivita na mauaji ya kimbari katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Sasa baada ya mahakama ya ICC kuituhumu serikali ya Marekani na kuitaja kuwa inabeba dhima ya jinai za wanajeshi na maafisa wake wa CIA huko nchini Afghanistan, tusubiri na kuona serikali ya Washington itachukua hatua gani kuhusiana na tuhuma hizo.

Baada ya tukio la Septemba 11 mwaka 2001, Rais wa wakati huo wa Marekani George W. Bush Oktoba mwaka 2001 alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi Afghanistan kwa kisingizo cha kupambana na ugaidi, ambapo mashambulio hayo yalipelekea kusambaratika utawala wa Taliban nchini humo.

Pamoja na hayo, kupelekwa majeshi ya Marekani nchini Afghanistan na baadaye kikosi cha Shirika la Kijeshi la NATO pamoja na hatua zilizochukuliwa na Washington, ni mambo yaliyoifanya Marekani iwe na faili jeusi kutokana na jinai na vitendo vilivyo dhidi ya binadamu vilivyofanywa na vikosi vyake huko Afghanistan. Hatua ya Marekani ya kuanzisha jela kubwa katika kambi ya kikosi cha anga ya Bagram na kuwatesa mamia ya raia wa Afghanistan kwa tuhuma ya kufanya vitendo vya kigaidi au kuwa na nia ya kufanya ugaidi, ni mambo ambayo kwa hakika yaliifanya Marekani ikabiliwe na kashfa kubwa ambayo daima imekuwa ikijidai kuwa kinara wa kutetea haki za binadamu.

George W. Bush akiwa Rais wa Marekani  wakati huo alitoa amri ya kushambuliwa kijeshi Afghanistan

Akthari ya wafungwa hao hata hawakuwa wakifahamu sababu ya kushikiliwa kwao na vikosi vya Marekani. Aidha wengi wa wafungwa hao walikabiliwa na miamala mibaya kama mateso na kuadhibiwa sambamba na kuvunjiwa heshima matukufu yao. Januari mwaka 2012 Kamati ya Kisheria ya serikali ya Afghanistan  ambayo iliundwa na Rais wa wakati huo wa nchi hiyo Hamid Karzai kwa ajili ya kuchunguza hali ya wafungwa, ilifichua jinai kubwa zilizofanywa na askari wa Marekani dhidi ya wafungwa katika gereza hilo la Bagram.

Ufuatiliaji huo wa kisheria umeandaa mazingira mazuri ya kukusanywa taarifa muhimu na zinazohitajika na katika hatua iliyofuata kufuatiliwa jinai hizo na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Tags