Feb 26, 2016 16:20 UTC
  • Hali mbaya ya wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain

Matukio yanayojiri nchini Bahrain yanaonyesha kuwa utawala wa Aal Khalifa unazidisha hatua za ukandamizaji dhidi ya wananchi kiasi kwamba kuwatia nguvuni na kuwafungulia kesi wanaharakati wa kisiasa kunazidi kuchukua sura pana zaidi inayozidi kutia wasiwasi siku baada ya siku.

Ripoti kutoka nchini humo zinaeleza kuwa kumeanza duru mpya ya utoaji hukumu za kidhalimu dhidi ya wanaharakati wa kisiasa, sambamba na utawala wa Aal Khalifa kuendeleza siasa zake za kidikteta kuhusiana na kuwaweka mahabusu wanaharakati wa kisiasa na viongozi wa mapambano ya wananchi; hali ambayo imeibua wimbi kubwa la malalamiko ya wafungwa wa kisiasa nchini humo.

Kuhusiana na suala hilo, makumi ya wafungwa wa kisiasa wamepoteza fahamu kutokana na mgomo wa kususia kula. Shirika la Ulaya na Bahrain la haki za binadamu limetangaza kuwa wafungwa 30 wa kisiasa wanaoshikiliwa kwenye jela ya Alhawdhul-Jaf wamepoteza fahamu kwa sababu ya kususia kula; na hali zao ni mbaya sana.

Tangu ulipoanza ukandamizaji wa vuguvugu la mapambano ya wananchi lililoanza mwaka 2011 hadi sasa, Bahrain inaendelea kushuhudia wimbi kubwa la malalamiko na upinzani wa umma unaotaka marekebisho ya kisiasa yafanyike nchini humo. Kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na maafisa usalama wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) waliotumwa nchini humo kupitia Kikosi cha Ngao ya Peninsula, pamoja na askari wa nchi nyengine kadhaa za Kiarabu walioko nchini humo, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kuzima sauti ya malalamiko ya wananchi hao. Kuendelea kutoa hukumu za kidhalimu na kionevu dhidi ya wanaharakati wa kisiasa kunafanywa katika hali ambayo kwa mujibu wa makundi ya upinzani hivi sasa kuna zaidi ya wapinzani 10,000 wa kisiasa katika jela za utawala wa Aal Khalifa; ambapo 150 miongoni mwao wamehukumiwa vifungo vya maisha, 150 ni watoto wadogo na mahabusu 150 wengine wamepoteza viungo vya mwili kwa mateso na ukatili waliofanyiwa na askari wa utawala huo.

Kuongezeka idadi ya wafungwa wa kisiasa nchini Bahrain kumewatia wasiwasi walimwengu, kwa sababu kutokana na ukiukaji huo mkubwa wa haki za binadamu na ukandamizaji wa matakwa halali ya wananchi, utawala wa Aal Khalifa umeigeuza Bahrain kuwa jela na gereza kubwa. Tangu tarehe 14 Februari mwaka 2011, wakati lilipoanza vuguvugu la mapinduzi ya wananchi hadi sasa, utawala wa Manama haujaacha kuchukua kila hatua kandamizi ikiwemo ya kuwafunga jela wanamapinduzi, viongozi wa upinzani pamoja na wananchi wanaoshiriki kwenye maandamano ya amani.

Mwenendo wa utawala wa Aal Khalifa unaonyesha kuwa sio tu utawala huo wa kiimla unawanyima uhuru wa kisiasa wananchi wa Bahrain bali pia unakandamiza hata haki zao nyengine za msingi zikiwemo za uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Siasa za utawala wa Aal Khalifa zimesimama juu ya msingi wa kuzidi kuvunjia heshima itikadi za wananchi wa Bahrain hususan za Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao ndio wanaounda sehemu kubwa ya jamii ya nchi hiyo.

Ili kuhakikisha unazima wimbi la malalamiko ya wananchi, utawala wa Kifalme nchini Bahrain umewatia nguvuni wanaharakati wengi wa kisiasa wanaoupinga utawala huo; na kwa kuwazushia kesi za kubuni kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela. Utawala wa Aal Khalifa unatumia kisingizio cha sheria ya kupambana na ugaidi ili kuzidisha mbinyo dhidi ya wapinzani na kushadidisha siasa za kipolisi nchini humo. Kwa mujibu wa sheria hiyo utawala huo wa kifamilia umejipa mamlaka ya kukandamiza mjumuiko wowote ule wa watu, kumkamata mpinzani yoyote kwa kisingizio eti ca kuunga mkono ugaidi na kulipiga marufuku kundi au harakati yoyote ile kwa kisingizio hicho hicho cha kuunga mkono ugaidi. Hayo yote yanajiri katika hali ambayo kutokana na uungaji mkono mkubwa unaopata kwa madola ya Magharibi na baadhi ya tawala za Kiarabu na unaopewa msukumo na kimya cha Jamii ya Kimataifa, utawala wa kiimla wa ukoo wa Aal Khalifa unaendeleza jinai zake dhidi ya wananchi wa Bahrain bila ya hofu wala wasiwasi wowote.../

Tags