Israel imeua watoto 41 Wapalestina kwa muda wa miezi mitano
Utawala haramu wa Israel umeua watoto 41 Wapalestina katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu katika kipindi cha miezi mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Watoto Tawi la Palestina (DCIP), idadi hiyo inajumuisha Wapalestina 31 waliokuwa chini ya umri wa miaka 18 ambao jeshi la Israel linadai walikuwa wakitekeleza mashambulizi ya visu au bunduki. DCIP inasema idadi hiyo haikujumlisha mtoto wa miaka 2 ambaye aliuawa pamoja na mama yake aliyekuwa na mimba wakati nyumba yao ilipolengwa na ndege za kivita za Israel katika Ukanda wa Ghaza. DCIP imeukosoa vikali utawala wa Kizayuni wa Israel kwa sera yake ya kuwapiga risasi kwa lengo la kuwaua watoto wa Palestina.
Tangu ilipoanza Intifadha ya Quds mwezi Oktoba 2015 hadi hivi sasa, wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wameshawaua shahidi Wapalestina zaidi 185 na kuwajeruhi wengine wengi.
Kwa upande wao Wapalestina wamejibu jinai hizo za Israel kwa kuangamiza Wazayuni 32 hadi hivi sasa na kujeruhi wengine wengi.