Mar 23, 2017 15:25 UTC
  • Syria yalalamikia kushadidi jinai za Marekani

Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria katika kulalamikia jinai za muungano wa Marekani wa eti kupambana na magaidi wa ISIS au Daesh, imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake na kusitisha mauaji ya raia na uharibifu unaofanywa na muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani nchini Syria.

Katika  barua mbili tofuati kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Baraza la Usalama, Wizara ya Mambo ya Nje ya Syria imesema: "Majeshi ya anga ya muungano wa kimataifa unaoongozwa na Marekani umehusika na mauaji mapya ya raia kwa kudondosha mabomu katika shule moja katika eneo la Al Mansura mjini Raqqa ambapo watoto zaidi ya 32 na mwanamke moja wameuawa na makumi ya raia kujeruhiwa sambamba na kuharibiwa kabisa shule hiyo."

Jinai hiyo ya muungano wa Marekani pamoja na ukatili unaofanywa na makundi kama vile ISIS na Jabhatu Nusra pamoja na makundi husika, ni mambo ambayo yamesababishia masaibu na uharibifu mkubwa watu wa Syria.

Kwa hakika harakati za Marekani na zile za magaidi zinasaidiana katika kushadidisha mauaji ya watu wa Syria.

Uharibifu wa vita vya Syria

Marekani, kwa njia ya moja kwa moja au kupitia muungano inaouongoza, inakiuka mamlaka ya kujitawala Syria kwani wakuu wa Damascus hawajatoa idhini kwa Washington kujihusisha kijeshi nchini humo.

Chokochoko za Marekani nchini Syria zinafanyika kwa misingi kadhaa kama vile kudai kutaka kurejesha utulivu na amani katika eneo la Mashariki ya Kati na eti kupambana na ugaidi. Hatua hizo za Marekani zimechangia katika kuzidisha mgogoro na mapigano Mashariki ya Kati au Asia Magharibi.

Halikadhalika uingiliaji wa kijeshi Marekani ulihitajia kibali cha Baraza la Usalama la Umoja wa Maaifa, lakini rais aliyeondoka wa Marekani alifuata nyayo za waliomtangulia na kuunda muungano eti dhidi ya ISIS, na kutumia nguvu za kijeshi Syria pasina idhini ya Baraza la Usalama.

Kuendelea ukiukwaji sheria huo ni jambo litakalokuwa na matokeo mabaya katika mfumo wa kimataifa na kutishia amani na usalama duniani.

Hivi sasa katika kipindi cha urais wa Donald Trump, uingiliaji kijeshi Marekani huko Syria unazidi kushadidi.

Hakuna shaka kuwa, kujichukulia sheria mkononi na kuchukua hatua zozote pasina kuzingatia sheria za kimataifa na kwa kukiuka mamlaka ya kujitawa nchi hakuwezi kukubalika hata kama ni kwa kisingizio cha kupambana na ISIS. Marekani inatumia kisingizio hicho kuwaua raia na kufanya jinai za kivita nchini Syria.

Nukta ya kutaamali hapa ni kuwa, Marekani imewasilisha mipango yenye kupotosha fikra za umma kama vile kuanzisha eti maeneo salama nchini Syria na Iraq ili kuweza kuingilia zaidi mambo ya ndani ya nchi hizo mbili na hivyo kupata mwanya wa kujipenyeza zaidi na kuendelea kuyaunga mkono makundi ya kigaidi ili yasishindwe kikamilifu. Baada ya kupata pigo kubwa magaidi huko Syria katika miezi ya hivi karibuni, mipango hiyo ya Marekani imeanza kusambaratika hasa  katika mji wa Aleppo ambapo magaidi walitimuliwa kikamilifu. Hivi sasa mkondo wa kuwaangamiza magaidi kikamilifu huko Syria umeshika kasi na jambo hilo limewatia wasiwasi mkubwa waungaji mkono wao hasa Marekani na waitifaki wake. Ni kwa sababu hiyo ndio maana waungaji mkono hao wa magaidi wakaanza kutumia kila mbinu ili kuwanusuru.

Magaidi watenda jinai wa ISIS wanaopata himaya ya Marekani

Ni wazi kwamba pamoja na kuwa Marekani imedia inataka kuwepo maeneo salama Syria kwa ajili ya wakimbizi na wanafunzi lakini ukweli wa mambo ni kuwa hakuna eneo lolote nchini humo lililosalimika na jinai na hujuma za Marekani.  Kupitia mipango yake ya kuhadaa fikra za waliowengi, Marekani inaandaaa mazingira ya kushadidisha jinai zake sambamba na kuwapa magaidi fursa ya kujiimarisha ili wakithirishe jinai zao nchini Syria.

Kuongezeka mashambulizi ya muungano wa Marekani unaodai kupambana na ISIS nchini Syria katika kipindi hiki cha kufanyika mazungumzo mapya ya utatuzi wa kisiasa wa  mgogoro wa Syria huko Geneva ni jambo linaloashiria sera zilizojaa shari za Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati. Muungano huo wa Marekani unalenga kuvuruga mazingira ya kisiasa yaliyojitokeza kwa ajili ya mazungumzo ya kutafuta utatuzi wa mgogoro wa Syria. Hakuna shaka kuwa, uvurugaji wa Marekani dhidi ya jitihada za kumatiafa za kutatua mgogoro wa Syria umeingia katika kipindi hatari zaidi.

Tags