Apr 16, 2017 12:16 UTC
  • Utupiaji jicho jinai za Israel katika kuwachukua mateka Wapalestina

Jumuiya ya Masuala ya Mateka na Watu Walioachiliwa Huru ya Palestina imetangaza kuwa, idadi ya mateka wa Kipalestina wanaoshikiliwa katika korokoro za utawala ghasibu wa Israel imefikia 6,500.

Taarifa ya pamoja iliyotolewa leo Jumapili na Jumuiya ya Masuala ya Mateka na Watu Walioachiliwa Huru ya Palestina na Kituo cha takwimu cha Palestina imeeleza kuwa, kati ya mateka Wapalestina 6,500, wanawake ni 57, watoto 300 na Wabunge 13. 

Taarifa hiyo imetolewa sambamba na kukaribia tarehe 17 Aprili ambayo inajulikana kwa jina la "Siku ya Mateka wa Kipalestina". Takwimu hizo zinatolewa katika hali ambayo, mateka wa Kipalestina wanafanya juhudi za kufanya mgomo wa pamoja. Katika miezi ya hivi karibuni Wapalestina wakiwa na lengo la kulalamikia hali mbaya na hatari ambayo imeandaliwa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina katika magereza ya utawala huo ghasibu na sisitizo lao la kuondoka katika magereza ya Israel, mara chungu nzima wamefanya migomo. Tangu utawala haramu wa Israel ulipoikalia kwa mabavu Palestina mnamo mwaka 1948 hadi hii leo, takribani Wapalestina milioni moja wametiwa mbaroni na kwa muktadha huo, Wapalestina wapatao milioni moja wamewahi kushikiliwa kwa muda katika jela za Israel.

Wanajeshi wa Israel wakimburuza Mpalestina

Hivi sasa sambamba na kukaribia tarehe 17 ambayo huadhimishwa kama Siku ya Mateka wa Kipalestina, Jumuiya ya Masuala ya Mateka na Watu Walioachiliwa Huru ya Palestina na ile ya Kituo cha Takwimu cha Palestina zimetoa taarifa ya pamoja na kutangaza kuwa, kadhia ya mateka wa Kipalestina ni miongoniu mwa misingi na nguzo muhimu za Wapalestina na kwamba, katika Intifadha ya 1987 na Intifadha ya Quds ya mwaka 2000 mamia ya maelfu ya Wapalestina walichukuliwa mateka.

Siku zote utawala haramu wa Israel umekuwa ukishadidisha hatua zake za kuwakamata mateka wa Palestina ili kuzusha hofu na wahaka miongoni mwa Wapalestina na hivyo kuwafanya waachane na hatua zao za kuendeleza muqawama na mapambano. Hapana shaka kuwa, hatua zote hizo za Israel zinabainisha kwamba, utawala huo uko tayari kufanya jambo lolote na jinai yoyote ile ili kutimiza muradi na malengo yake. Ushahidi wa hilo ni jinai na ukandamizaji usiokoma wa utawala huo pamoja na dhulma kubwa ya kila leo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Katika mazingira kama hayo, mateka wa Kipalestina wamekuwa wakifanya mgomo wa kula ili kwa njia hiyo, wawafikishie walimwengu sauti yao ya kudhulumiwa. Aidha hatua ya Wapalestina hao imepepelekea kuibuka makabaliano baina yao na Israel na hivyo kuyageuza magereza ya utawala huo ghasibu kuwa mahala pia pa mapambano ya kudumu dhidi ya Wazayuni maghasibu.

Haya ni baadhi ya mateso ya wanajeshi wa Israel kwa vijana wa Kipalestina

Katika miaka ya hivi karibuni, mateka wa Kipalestina wameweza kuonyesha sura halisi ya utawala haramu wa Israel mbele ya macho ya walimwengu, jinsi ulivyokiuka wazi kabisa vipengee vya mkataba wa Geneva.  Jambo hilo limezidi kuumbua zaidi utawala wa Israel ulimwenguni. Harakati ya malalamiko ya mateka wa Kipalestina siku zote imekuwa ikiambatana na wimbi la harakati za upinzani za wananchi wa Palestina katika kuwaunga mkono mateka wa Kipalestina dhidi ya utawala huo ghasibu. Malalamiko hayo yamekuwa yakipelekea kushadidi Intifadha ya wananchi wa Palestina, jambo ambalo linabainisha juu ya kuweko mkakati wa Wapalestina wa kuanzisha Intifadha mpya kwa msingi wa mateka wa Kipalestina.

Katika mazingira haya, suala la kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina limekuwa likihesabiwa kuwa miongoni mwa mambo ya msingi katika mkondo wa mapambano ya Wapalestina. Hatua ya Wapalestina ya kusisitiza kufungamana kwao na mateka wa Kipalestina katika minasaba na matukio mbalimbali kama Siku ya Mateka wa Kipalestina imewathibitisha walimwengu kwamba, kamwe hawatalegeza kamba katika kukabiliana na maghasibu wa Kizayuni.

Fikra za waliowengi ulimwenguni zina matarajio kwamba, mwaka huu yaani 2017 uwe ni mwaka wa kuachiliwa huru mateka wa Kipalestina. Ili kutimia hilo, jumuiya na asasi za kimataifa zinapaswa kuchukua hatua za maana kuwaunga mkono mateka wa Kipalestina na kwa juhudui za Wapalestina za kuachiliwa huru mateka wao kutoka katika magereza ya kuogofya ya Israel walimwengu wasishuhudie tena mauaji ya mateka hao katika jela za utawala haramu wa Israel.

Tags