Oct 04, 2024 07:13 UTC
  • Israel yaendelea kumwaga damu za Walebanon mjini Beirut

Wizara ya Afya ya Lebanon imesema takriban watu 37 wameuawa shahidi huku wengine zaidi ya 150 wakijeruhiwa katika mashambulizi mapya ya anga ya utawala haramu wa Israel, huku uchokozi usio na kikomo wa utawala huo katili dhidi ya Lebanon ukiendelea.

Wizara ya Afya ya Lebanon imesema katika taarifa ya usiku wa kuamkia leo Ijumaa kuwa, "Mashambulizi ya adui Mzayuni katika saa 24 zilizopita yameua watu 37 na kujeruhi 151." 

Habari zaidi zinasema kuwa, Israel ilianzisha mashambulizi kadhaa ya anga kwenye kitongoji cha Beirut kusini mwa Dahiyeh siku ya Alhamisi.

Utawala huo ulitumia mabomu yenye nguvu zaidi katika mashambulizi yake ya hivi punde, ambayo idadi yake ilikuwa zaidi ya dazeni moja. Majengo kadhaa ya raia yalilengwa kwenye mashambulizi hayo ya hivi karibuni ya utawala pandikizi wa Israel.

Ripoti zinaonyesha kuwa, mabomu zaidi yalitumika katika mashambulizi ya hivi punde zaidi ikilinganishwa na hujuma iliyomuua shahidi, Kiongozi wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, Ijumaa iliyopita. Mashambulizi hayo pia yalipiga karibu na uwanja wa ndege wa kimataifa wa Beirut.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Kizayuni, kuuawa kwa Hashem Safieddine, Mkuu wa Baraza Kuu la Hizbullah, ndilo lilikuwa lengo kuu la mashambulizi ya utawala huo ghasibu.

Kwa mujibu wa data za serikali ya Lebanon, idadi ya vifo kutokana na mashambulizi ya anga ya Israel katika maeneo mbali mbali ya Lebanon tangu mapema Oktoba 2023 imepindukia watu 1,700, huku wengine karibu 8,770 wakijeruhiwa.

Tags