Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Usitishaji vita Lebanon na Gaza unapaswa kufanyika kwa wakati mmoja
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, Iran inaunga mkono usitishaji vita kwa sharti kwamba, haki za wananchi wa Lebanon ziheshimiwe na kukubaliwa na Muqawama na kusema: Usitishaji huo wa mapigano unapaswa kuwa sawia na usitishaji vita huko Gaza.
Sayyid Abbas Araghchi, ameyasema hayo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Beirut huko Lebanon na kuongeza kuwa, Iran itasimama upande wa Lebanon na Muqawama, na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel zitashindwa kama ilivyokuwa huko nyuma. Araghchi amesisitiza kuwa shindi utakuwa wa taifa la Lebanon.
Kuhusiana na mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekumbusha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu haikuanzisha mashambulizi hayo, bali ilijibu mashambulizi ya Israel dhidi ya ardhi na ubalozi wa Iran mjini Damascus na mashambulizi dhidi ya malengo ya Iran; na tofauti na Wazayuni, ambao walilenga watu na makazi ya raia na kushambulia wanawake na watoto, Iran imeshambulia tu vituo vya kijeshi na usalama vya utawala wa Kizayuni.

Sayyid Abbas Araghchi ameongeza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu haina nia ya kuendeleza mashambulizi, lakini kama utawala wa Kizayuni utaendeleza mashambulizi na kuchukua hatua nyingine yoyote dhidi ya Iran, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali, sawia na la mahesabu maalumu.
Ujumbe wa kidiplomasia wa Iran ukiongozwa na Sayyid Abbas Araghchi uliwasili Beirut jana kwa ajili ya kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa Lebanon na pia kuwasilisha shehena ya tani 10 za chakula na dawa kama sehemu ya misaada ya kibinadamu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa watu wa nchi hiyo walioathiriwa na mashambulizi ya kikatili ya Israel.