Wazayuni washambulia kwa makombora uwanja wa ndege Damascus, Syria
Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya shambulizi la anga dhidi ya uwanja wa ndege wa Damascus nchini Syria, wiki tatu baada ya Marekani kutekeleza hujuma kama hiyo ya kichokozi.
Shirika la habari la Al-Masdar la Syria limeripoti kuwa, uwanja huo wa kimataifa wa ndege umetikiswa kwa mashambulizi matano ya anga, yanayoaminika kufanywa na ndege za kivita za Israel.
Kadhalika kanali ya televisheni ya Al-Manar ya Lebanon imethibitisha kutokea wimbi hilo la mashambulizi ya anga dhidi ya uwanja wa ndege wa Damascus na kuongeza kuwa, kituo cha kuhifadhi silaha pambizoni mwa uwanja huo pia kimeshambuliwa na kuharibiwa.
Rami Abdulrahman, Mkuu wa shirika linalojiita Syrian Observatory for Human Rights amesema sauti kubwa za milipuko zimesikika katika sehemu kubwa ya mji wa Damascus kufuatia hujuma hiyo ya anga.
Ndege za kijeshi za utawala pandikizi wa Israel zimekuwa zikilenga viwanja vya ndege na kambi za jeshi mjini Damascus, huku shambulizi la leo likishabihiana na lile lililofanywa na utawala huo bandia Disemba mwaka 2014.
Si vibaya kukumbusha hapa kuwa, tarehe 7 mwezi huu wa Aprili, Marekani ilifanya shambulio la makombora yake ya Tomahawk dhidi ya kituo cha jeshi la anga la Syria huko Shayrat kwa madai kuwa Syria imetumia silaha za kemikali katika vita vyake dhidi ya magaidi.
Shambulio hilo la Marekani lilifanyika hata kabla ya kufanyika uchunguzi kuhusu madai hayo bandia, ambayo serikali ya Rais Bashar al-Assad imeyakanusha vikali.