May 14, 2017 03:40 UTC
  • Mapigano yashtadi kati ya makundi ya kigaidi mjini Idlib nchini Syria

Sambamba na kukaribia kwa duru mpya ya mazungumzo ya Geneva kuhusiana na mgogoro wa Syria, mapigano yameshtadi kati ya makundi ya wabeba silaha katika mji wa Idlib, kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.

Mapigano hayo baina ya makundi ya upinzani dhidi ya serikali yameibuka baada ya kundi la kigaidi la Ahraru sh-Sham lenye mafungamano na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Jab'hatu Nusra kushambulia na kudhibiti baadhi ya ngome na maghala ya kuhifadhia silaha ya wapiganaji wa kundi linalojiita 'Jeshi Huru la Syria.'

Magaidi wanaouana na kufanya jinai Syria

Katika hujuma ya kundi hilo, inaelezwa kuwa wapiganaji wa kundi la Ahraru sh-Sham walimuua pia kiongozi wa kundi la Jeshi Huru la Syria. Habari zaidi zinasema kuwa, hatua ya kufikiwa makubaliano ya hivi karibuni ya Astana mji mkuu wa Kazakhstan kwa ajili ya kuanzishwa maeneo salama nchini Syria na kadhalika kukaribia duru mpya ya mazungumzo ya Geneva juu ya mgogoro wa nchi hiyo, kumepelekea makundi ya kigaidi kupigana vikali katika mji wa Idlib.

Mchoro unaoonyesha uhalisia wa makundi yanayogigana huko Syria

Katika mapigano hayo makumi ya wapiganaji wa pande mbili waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Inafaa kuashiria kuwa kushindwa mtawalia kwa makundi ya kigaidi nchini Syria na kadhalika kusonga mbele kwa jeshi na harakati ya muqawama dhidi ya magaidi, kumeibua tofauti kubwa baina ya viongozi wa makundi ya kigaidi na hivyo kuanza kushambuliana.

Tags