May 26, 2017 07:30 UTC
  • Wabahrain waendeleza maandamano ya kulaani udhalimu wa ufalme wa nchi hiyo

Wananchi wa Bahrain wameendeleza maandamano ya kitaifa ya kulaani udhalimu na umwagaji damu unaoendelezwa na utawala wa Aal Khalifa katika kijiji cha Diraz ambacho ni makao ya mwanazuoni maarufu wa Kiislamu Sheikh Isa Qassim.

Leo Ijumaa kunatazamiwa kufanyika maandamano makubwa kote Bahrain baada ya sala ya Ijumaa kama ambavyo jana Alkhamisi pia wananchi wenye hasira walimiminika mitaani kulaani hatua ya jeshi la Bahrain ya kuvamia nyumba ya Sheikh Isa Qassim na kuwaua Waislamu watano katika hujuma hiyo.

Katika maandamano ya jana, watu tisa walikamatwa wakati wanajeshi walipotumia nguvu ziada kuwatawanya waandamanaji.

Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa kiroho wa chama cha Kiislamu cha Al Wefaq yuko katika kifungo cha nyumbani baada ya kupokonywa uraia mwezi Juni mwaka jana.

Aidha Jumapili alihukumiwa kifungo cha nyumbani cha mwaka moja kwa kosa la kukusanya Khums huku utawala wa Bahrain ukichukua udhibiti wa mali za Waislamu zenye thamani ya dola milioni nane ambazo alikuwa akizisimamia.

Maandamano ya kumuunga mkono Sheikh Isa Qassim

Leo wananchi wa Iran wanajiunga na Waislamu wa maeneo mengine duniani katika maandamano ya kulaani udhalimu anaotendewa Sheikh Isa Qassim.

Tokea tarehe 14 Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa ikishuhudia harakati ya mwamko wa Kiislamu dhidi ya ukandamizaji na mbinyo wa watawala wa ukoo wa Aal Khalifa. Wananchi hao wanataka kuweko uhuru, uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuingia madarakani serikali iliyochaguliwa na wananchi. 

Utawala huo ukiwa na lengo la kuzima sauti na cheche za moto wa malalamiko hayo umewatia mbaroni wanaharakati wa kisiasa, vijana na raia wengine wa nchi hiyo na kuwahukumu vifungo vya muda mrefu jela.

Tags