Iran: Tunaunga mkono mwenendo wa amani nchini Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i29788-iran_tunaunga_mkono_mwenendo_wa_amani_nchini_afghanistan
Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan ametangaza kuunga mkono kikao cha mjini Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo chenye lengo la kudumisha usalama ndani ya taifa hilo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
May 30, 2017 03:41 UTC
  • Iran: Tunaunga mkono mwenendo wa amani nchini Afghanistan

Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Afghanistan ametangaza kuunga mkono kikao cha mjini Kabul, mji mkuu wa nchi hiyo chenye lengo la kudumisha usalama ndani ya taifa hilo.

Itakumbukwa kuwa tarehe 20 ya mwezi huu, Rais Ashraf Ghani wa Afghanistan alikutana na mabalozi wa nchi za kigeni wanaoishi mjini Kabul na kutangaza kuwa mwezi ujao wa Juni kutafanyika kikao kilichopewa jina la 'Mwenendo wa Kabul' kwa kuhudhuriwa na nchi za eneo kwa ajili ya kudumisha usalama. Katika kikao hicho serikali ya Afghanistan imekusudia kuwasilisha mapendekezo yatakayowavuta wanachama wa kundi la Taleban kwenye meza ya mazungumzo huku msingi mkuu wa mazungumzo hayo ukiwa ni amani ya taifa hilo.

Viongozi wa pande mbili

Balozi wa Iran nchini Afghanistan, Mohammadreza Bahrami amekutana na Hekmat Khalil Karzai, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Afghanistan katika masuala ya kisiasa na kumuhakikishia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono juhudi zozote zenye lengo la kudumisha usalama na amani nchini humo na kwamba katika suala hilo, Tehran haitosita kutoa ushirikiano. Kwa upande wake Hekmat Khalil Karzai amemueleza balozi wa Iran mwenendo wote wa mazungumzo hayo tarajiwa ya 'Mwenendo wa Kabul.' Kadhalika pande mbili mbali na kuonyesha kufurahishwa na mahusiano ya Iran na Afghanistan katika nyanja tofauti zimesisitiza juu ya udharura wa kusonga mbele kwenye mashirikiano zaidi na ya pande zote.