Jun 17, 2017 15:33 UTC
  • Qatar yaomba msaada wa Umoja wa Mataifa

Mkuu wa Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar katika ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi ameuomba umoja huo uingilie kati na kutatua mgogoro ulioanzishwa na Saudia, Imarati, Bahrain na Misri dhidi ya nchi yake.

Jumatatu ya tarehe 5 Juni, 2017, nchi za Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu yaani Imarati, Bahrain na Misri zilikata uhusiano wao wa kila upande na Qatar. Nchi za Saudia, Imarati na Bahrain zina mipaka ya majini na angani huku Saudia ikiwa pia na mpaka wa ardhini na Qatar. Nchi hizo zimekata uhusiano wao katika mipaka yao yote na nchi hiyo ndogo ya Kiarabu.

Ali Bin Samikh al Marri, mkuu wa Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar

 

Televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon leo imemnukuu Ali Bin Samikh al Marri, mkuu wa Kamati ya Taifa ya Haki za Binadamu ya Qatar akisema leo mbele ya waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kwamba, kama mzingiro huo dhidi ya nchi yake hautakomeshwa, kuna uwezekano Doha ikaitaka ofisi moja ya wakala wa kimataifa kufuatilia kulipwa fidia na pia kutumia taasisi za kisiasa kutetea haki zake.

Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, hatua ya Qatar ya kuuomba Umoja wa Mataifa uingilie mgogoro ulioanzishwa dhidi yake na Saudi Arabia, ina maana ya kwamba Doha imeamua  kusimama imara na kupambana na Riyadh kwa nguvu kubwa zaidi.

Habari nyingine inasema kuwa, gazeti la al Sharq linalochapishwa nchni Qatar limenukuu makala iliyoandikwa na Faisal Qassim mmoja wa waandishi maarufu katika ulimwengu wa Kiarabu akisema kuwa, Marekani imeamua kuwachochea Waarabu wauane wenyewe kwa wenye ili ipate fursa ya kupora utajiri wao. 

Tags