UNICEF: Watoto wa Iraq wanaendelea kuteseka kwa vita
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i30832-unicef_watoto_wa_iraq_wanaendelea_kuteseka_kwa_vita
Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kwamb, watoto takriban milioni tano nchini Iraq wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 22, 2017 11:45 UTC
  • UNICEF: Watoto wa Iraq wanaendelea kuteseka kwa vita

Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umetahadharisha kwamb, watoto takriban milioni tano nchini Iraq wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu.

Shirika hilo limesema katika taarifa yake kwamba, watoto wa nchi hiyo hususan wale wote walioko katika mji wa Mosul, ambako majeshi ya Iraq yanapambana vikali na kundi la kigaidi la Daesh, wamejikuta katika ghasia na umasikini usio na kikomo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa, tabakala la watoto nchini Iraq limeendelea kuteseka kutokana na machafuko yanayoshuhudiwa katika nchi hiyo na kuwafanya watoto wakose huduma muhimu.

Takwimu za Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF zinaonesha kuwa, nusu ya wagonjwa wanaotibiwa katika vituo vya watu wenye maradhi ya wasiwasi na kuchanganyikiwa kutokana na hofu na magonjwa mabaya ya akili magharibi mwa Mosul ni watoto wadogo.

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF

Sehemu nyingine ya ripoti hiyo inasema kuwa, watoto wapatao laki nane nchini Iraq wamepoteza mzazi japo mmoja huku wakikabiliwa na hali mbaya kutokana na kukosekana usalama katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo.

Mashirika ya misaada yanasema fedha zaidi zinahitajika haraka kuweza kusaidia kuwalinda watoto wa Iraq, kutokana na mapigano hayo hususan katika maeneo ambayo kunashuhudiwa mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh.