Jun 25, 2017 15:45 UTC
  • Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki: Tutaendelea kuwa pamoja na Qatar

Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki sambamba na kuunga mkono msimamo wa Qatar kuhusu matakwa ya baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo la Ghuba ya Uajemi amesema kuwa, nchi yake itaendelea kuwa pamoja na Doha.

Rais Erdoğan aliyasema hayo baada ya swala ya Idul Fitr katika msikiti wa Mimar Sinan mjini Istanbul ambapo sambamba na kutoa salamu za siku kuu hiyo kwa raia wa nchi hiyo na Waislamu kwa ujumla, amepongeza hatua ya serikali ya Doha ya kupinga masharti 13 yaliyotolewa na nchi hizo za Kiarabu na kusema kuwa, hatua hiyo ni mwafaka.

Erdoğan alipofanya safari nchini Qatar

Kadhalika Erdoğan amesema kuwa, anayatambua masharti hayo kama ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa ambayo ni sawa na kushambulia haki ya kujitawala ya raia wa nchi husika, suala ambalo kimataifa halikubaliki. Ameongeza kuwa, pendekezo la kutaka kufungwa kambi ya kijeshi ya Uturuki na Qatar ni kuivunjia heshima Ankara na kusisitiza kuwa, Uturuki kamwe haitaomba idhini kutoka kwa nchi yoyote katika harakati zake za kujilinda. Rais Erdoğan amelaani vikali vikwazo vilivyowekwa na Saudia na baadhi ya nchi za Kiarabu dhidi ya Qatar na kusema kuwa, hivi sasa serikali ya Doha inakabiliwa na vikwazo tofauti na kwamba Ankara itaendelea kuiunga mkono nchi hiyo katika kukabiliana na vikwazo hivyo.

Wanajeshi wa Uturuki wametumwa Qatar 

Miongoni mwa masharti 13 ya Saudia, Imarati, Bahrain na Misri kuihusu Qatar, ni pamoja na kuitaka serikali ya Doha kukata mahusiano yake ya kidiplomasia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Hizbullah, harakati ya Palestina ya HAMAS, kusimamisha kikamilifu kanali za televisheni ya al-Jazeera na kuhitimisha mashirikiano ya kijeshi baina ya Qatar na Uturuki, masharti ambayo yametajwa na Doha kuwa yasiyoingia akilini.

Tags