Qatar yalaani ukaidi wa Saudia wa kukataa suluhu
Serikali ya Qatar imelaani ukaidi wa Saudi Arabia wa kukataa kufanya mazungumzo na Doha kwa ajili ya kutafuta njia za kuondoa vikwazo vya nchi nne za Kiarabu dhidi ya Qatar.
Shirika la habari la Ufaransa limemnukuu Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Aal Thani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar akisema leo Jumatano kwamba msimamo wa Saudia dhidi ya nchi yake haukubaliki kabisa kwani unakinzana na misingi inayotawala katika uhusiano wa kimataifa.
Ikumbukwe kuwa, jana Jumanne, Adel al Jubeir, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia alisisitiza kuwa, hakuna mazungumzo yoyote yanayoweza kufanyika kati yao na viongozi wa Doha kuhusu masharti yaliyotolewa na Saudia na wenzake kwa Qatar.
Al Jubeir alisema katika mtandao wa Tweeter kwamba, masharti ya Riyadh kwa Doha hayawezi kufanyiwa mazungumzo na kwamba Qatar haina chaguo jingine isipokuwa kutekeleza tu masharti hayo.
Mapema asubuhi siku ya Jumatatu ya tarehe 5 Juni, 2017, Saudia ilitangaza kukata uhusiano wake wote na Qatar, na hapo hapo kuwataka waitifaki wake wafuate mkondo huo. Muda mchache baada ya hatua hiyo ya Saudia, nchi nyingine za Bahrain, Misri na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) nazo zilifuata mkondo huo wa kukata uhusiano wao wa kila upande na Qatar kwa madai ya kuunga mkono ugaidi na kuingilia mambo ya nchi hizo madai ambayo yamekanushwa vikali na Doha.
Wiki iliyopita, Saudia iliipatia Qatar hati ya masharti 13 na kusema kuwa, uhusiano wake na Doha hauwezi kurejea katika hali ya kawaida kama masharti hayo hayajatimizwa. Miongoni mwa masharti hayo ni kuitaka Doha ikate uhusiano wake na Ikhwanul Muslimin, Harakati ya Mapambano ya Palestina HAMAS pamoja na Iran na pia ifunge kambi ya kijeshi ya Uturuki katika ardhi ya Qatar.