Saudi Arabia mwasisi wa vitendo vya uchupaji mipaka nchini Uingereza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31382-saudi_arabia_mwasisi_wa_vitendo_vya_uchupaji_mipaka_nchini_uingereza
Matokeo ya utafiti mpya wa hivi karibuni uliofanywa nchini Uingereza umeitaja Saudi Arabia kuwa mwanzilishi mkuu wa vitendo vya uchupaji mipaka nchini humo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 05, 2017 23:33 UTC

Matokeo ya utafiti mpya wa hivi karibuni uliofanywa nchini Uingereza umeitaja Saudi Arabia kuwa mwanzilishi mkuu wa vitendo vya uchupaji mipaka nchini humo.

Taasisi ya Henry Jackson iliyofanya utafiti huo imetangaza katika ripoti yake kuwa nchi kadhaa zinazopakana na Ghuba ya Uajemi zimekuwa na nafasi kuu katika kuenea misimamo na vitendo hivyo vya kufurutu ada kwa kutokana na kuvipa misaada ya kifedha baadhi ya vituo vya mafunzo ambavyo vilikuwa wenyeji wa waenezaji wa misimamo hiyo mikali. Kwa mujibu wa uchunguzi huo, Saudi Arabia ambayo ni kinara wa nchi hizo zilizotajwa, inaeneza imani potofu za misimamo ya kuchupa mipaka kwa kueneza aidiolojia ya taasubi ya Uwahabi. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, baadhi ya taasisi nchini Uingereza ambazo zinadhaminiwa bajeti yake na Saudi Arabia zimetuhumiwa moja kwa moja kuwa zinasimamiwa na kuendeshwa moja kwa moja na Saudi Arabia. Taasisi hiyo iliyofanya utafiti kuhusu uhusiano wa nje ya Uingereza imeitaka serikali ya London ifanye utafiti na kuchunguza nafasi ya Saudia katika kuunga mkono itikadi za uchupaji mipaka. 

Saudi Arabia na fikra ya kueneza Uwahabi nchini Uingereza  

Huu si uchunguzi wa awali kuwahi kufanywa nchini Uingereza kuhusu nafasi ya Saudi Arabia katika kuunga mkono kifedha na kueneza fikra za uchupaji mipaka na za kigaidi. Kabla ya kufanyika uchunguzi huu wa Taasisi ya Henry Jackson, kuliwahi kufanyika pia uchunguzi mwingine kuhusu waungaji mkono wa taasisi zinazoeneza vitendo vya misimamo mikali na kufurutu ada kwa amri ya David Cameroon, Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo na katika zama zile ambapo Bi Theresa May alikuwa akiongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza. Mtuhumiwa mkuu katika matokeo ya utafiti huo ilikuwa ni nchi ya Saudia. Hata hivyo Theresa May anapinga kuchapishwa matokeo rasmi ya uchunguzi huo licha ya kupita zadi ya mwaka mmoja tangu kumaliza uchunguzi.  Serikali ya Uingereza inapinga kuchapishwa matokeo ya uchunguzi uliotajwa kwa kuhofia taathira hasi zinazoweza kuathiri uhusiano wa karibu sana na kiistratejia kati ya Uingereza na Saudi Arabia iwapo waungaji mkono wa taasisi zinazoeneza vitendo vya uchupaji mipaka na ugaidi watawekwa wazi. 

David Cameroon, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza 

Tangu aingie madarakani huko Uingereza, Theresa May amekuwa akifuatilia suala la kuimarisha uhusuano wa nchi yake na nchi za Kiarabu za pambizoni mwa Ghuba ya Uajemi; ambapo safari yake ya kwanza mara baada ya kuanza mchakato wa kujiondoa Uingereza katika Umoja wa Ulaya ilikuwa ni ziara yake nchini Saudi Arabia; safari inayohesabiwa kuwa ni hatua kubwa ya kimaonyesho.  Kushindwa kuchapishwa ripoti hiyo inayoashiria uungaji mkono wa kifedha wa nchi ajinabi kwa makundi yenye misimamo mikali huko Uingereza, kulizusha makelele mengi katika siku za mwisho za uchaguzi wa bunge la nchi hiyo wa kabla ya wakati wake tarehe Nane mwezi Juni mwaka huu na baada ya kutokea mashambulizi ya kigaidi katika mji wa Manchester na katika daraja moja mjini London. Katika kipindi hicho cha uchaguzi, Tim Farron, Kiongozi wa chama cha Liberal Democrat alisema kuwa Cameroon aliwahi kusema kwamba ripoti hiyo itakuwa imetolewa hadi kufikia msimu wa machipuo mwaka jana wa 2016, hata hivyo muda mfupi baadaye Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uingereza ikatangaza kuwa huenda ripoti hiyo isichapishwe kamwe kutokana na muhtawa nyeti sana uliomo ndani ya ripoti hiyo. 

Bi Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza akiwa pamoja na viongozi wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi  

Naye Dan Jervis, mbunge wa chama cha Leba katika bunge la Uingereza ambaye anaunga mkono ripoti hiyo mpya ameeleza kuwa, uhusiano wa Saudia na uungaji mkono wake kwa makundi yenye misimamo mikali ni jambo linalotia wasiwasi sana. Mbunge huyo ameitaka serikali ya London ichapishe muhtawa na yote yaliyomo kwenye ripoti ya serikali kuhusu uungaji mkono wa nje, kwa taasisi kama hizo.