ISIS yakiri kuwa kiongozi wake Abubakar al Baghdadi ameshaangamizwa
Kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limetoa taarifa na kutangaza rasmi kuwa, mkuu wa genge hilo Abubakar al Baghdadi ameshaangamizwa
Mtandao wa habari wa al Sumaria News wa nchini Iraq umeripoti habari hiyo leo Jumanne na kuongeza kuwa, magaidi wa Daesh wametoa ujumbe mfupi unaothibitisha habari za kuuawa Abubakar al Baghdadi na kusema kuwa watateuta kiongozi mpya wa kushika nafasi ya al Baghdadi.
Chombo hicho cha habari cha Iraq kimeongeza kuwa, hadi siku mbili zilizopita, magaidi wa Daesh walikuwa wamepiga marufuku kutoa matamshi yoyote kuhusiana na kuuawa Abubakar al Baghdadi huko Tal Afar na hivyo ilitabiriwa kwamba karibuni hivi kundi hilo la wakufurishaji litathibitisha habari ya kuangamizwa al Baghdadi.
Televisheni ya al Alam imeunukuu mtandao huo wa habari wa Iraq ukisema kuwa, hatua ya genge la ISIS ya kutangaza habari ya kuuawa kiongozi wake al Baghdadi katika mazingira ya kimya kana kwamba haina umuhimu wowote, imezusha maswali mengi kati ya wanachama wa genge hilo la kigaidi hususan kwa kuzingatia kuwa, habari za kuuawa viongozi wengine wa Daesh zimekuwa zikipewa umuhimu mkubwa na genge hilo.
Siku ya Jumapili, Waziri Mkuu wa Iraq, Haidar al Abadi, alitangaza kupitia Tweeter habari ya kukombolewa mji wa Mosul na kushindwa genge la kigaidi la Daesh katika mji huo. Jana Jumatatu alitangaza rasmi kukobmolewa mji huo akiwa katikati ya eneo la kale la Mosul ambalo ndilo lililokuwa ngome kuu ya magaidi wa ISIS.