Hali ya kutoaminiana yatanda katika baraza la PGCC
Miongoni mwa matokeo na athari mbaya za mivutano iliyopo baina ya Qatar na kundi la Kiarabu la 3+1 yaani nchi tatu wanachama katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi (PGCC) pamoja na Misri, ni kushadidi hali ya kutoaminiana ndani ya baraza hilo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Mohammed bin Abdulrahman Al Thani amesema kuhusu taathira za mvutano uliopo baina ya nchi yake na kundi ya 3+1 kwa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kuwa: "Baraza hilo lilianzishwa kwa sababu za kistratijia na kwa msingi wa kuaminiana, lakini baada ya mgogoro wa sasa hali hiyo ya kuaminiana imetoweka na itachukua kipindi kirefu kuweza kuijenga tena".
Zimepita siku 70 tangu ulipoanza mgogoro wa nchi za Qatar na kundi la 3+1 ambazo ni wanachama watatu wa Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemini yaani Saudia, Imarati na Bahrain pamoja na Misri. Tarehe 5 Juni nchi hizo nne zilikataka uhusiano wao na Qatar kwa sababu ya kile kilichotajwa kuwa ni uungaji mkono wa Doha kwa makundi ya kigaidi na siasa zake zisizooana na sera za nchi hizo. Vilevile zilifunga mipaka yote ya nchi kavu, anga na baharini na Qatar ili kuilazimisha nchi hiyo ibadilishe siasa na misimamo yake ya kieneo. Kwa upande wake Qatar imepinga tuhuma hizo na kusema Saudi Arabia inaamiliana na nchi hiyo kikabe na kwamba zama hizo zimepita. Doha inasisitiza kuwa, nchi hizo zinapaswa kuheshimu mamlaka na kujitawala kwa Qatar. Msimamo huo wa Qatar umepanua zaidi mivutano ndani ya nchi za Kiarabu na kulidhoofisha Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi.
Kimsingi moja kati ya sababu kuu za mgogoro wa sasa kati ya nchi hizo za Kiarabu ni kwamba Saudi Arabia na washirika wake wawili yaani Imarati na Bahrain zinaamini kwamba, siasa zinazohusiana na masuala ya kikanda za Qatar hazioani na zile zinazotawala Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi. Kwa maneno mengine ni kuwa, nchi hizo zinaitaka Qatar ichukue maamuzi yake kuhusu siasa za kigeni kwa mujibu wa misimamo na mitazamo ya baraza la PGCC. Hata hivyo Qatar na kutokana na mienendo ya Saudi Arabia, imefikia natija kwamba, Riyadh inataka kulitumia Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi kama wenzo wa kutimizia malengo yake na kulazimisha matakwa yake kwa wanachama wengine wa baraza hilo. Kwa msingi huo Qatar imekuwa ikionekana katika migogoro mingi iliyojitokeza katika baraza la PGCC linalojumuisha nchi sita za Saudia, Kuwait, Bahrain, Umoja wa Falme wa Kiarabu (Imarati), Oman na Qatar.
Suala jingine la kuashiriwa hapa ni kuwa, Qatar si mwanachama pekee asiyekuwa na imani tena na Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi. Nchi za Kuwait na Oman pia zimekataa kufuata maamuzi yanayochukuliwa na Saudi Arabia katika baraza hilo. Kwa mfano tu, nchi hizo mbili zimekataa kukata uhusiano wao na Qatar katika mgogoro wa sasa kati ya nchi hiyo na Saudi Arabia. Suala hilo limepelekea kujitokeza mgawanyiko katika baraza la PGCC.
Ni kwa sababu hiyo ndipo Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar akasema kuwa, hali ya kuaminiana imetoweka katika Baraza la Ushirikiano wa Ghuba ya Uajemi. Inatupasa kuelewa kwamba, kutawala anga ya kutoaminiana katika jumuiya yoyote huwa na maana ya "kifo" cha jumuiya hiyo. Hii ni kwa sababu, sharti muhimu la ufanisi wa jumuiya yoyote ya kikanda ni kuwepo maelewano na mazingira ya kuaminiana kati ya wanachama wake, suala ambalo halionekani katika kipindi chasa kwenye jumuiya hiyo.