Iran na Uturuki, udharura wa ushirikiano wa kiusalama
Meja Jenerali Mohammad Baqeri, Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye yuko safarini nchini Uturuki amesema kuwa, nchi hizo mbili zimeazimia kuzidisha uhusiano na ushirikiano katika pande zote hususan katika masuala ya kijeshi na kiulinzi.
Meja Jenerali Mohammad Baqeri, amewaambia waandishi wa habari mjini Ankara baada ya mkutano wake na Rais wa Uturuki, Recep Teyyip Erdogan na vilevile mwenyeji wake, Hulusi Akar kuwa, masuala ya kieneo, kupambana na zimwi la ugaidi na ushirikiano wa kulinda mipaka ni katika mambo yaliyozungumzwa katika mkutano wa pande hizo mbili.
Japokuwa mitazamo ya Tehran na Ankara kuhusiana na masuala ya kikanda inatofautiana na pengine kupinga, lakini pande hizo mbili zinakutana na kuafikiana katika suala la kupambana na ugaidi na haja ya kulindwa kwa pamoja usalama wa eneo hili. Vivyo hivyo, Iran na Russia hazina msimamo na mitazamo sawa kuhusiana na masuala mengi ya kikanda lakini nchi hizo mbili zinaafikiana katika masuala muhimu kama vile kuhusu kadhia ya kulindwa amani na usalama na udharura wa kupambana na ugaidi. Ushirikiano huo wa Iran na Russia katika masuala ya usalama umesadia sana kupeleka mbele gurudumu la mazungumzo ya kutafuta suluhisho la mgogoro wa Syria, na sasa mazungumzo ya Astana yanayofanyika sambamba na mafanikio yaliyopatikana katika medani za vita dhidi ya magaidi wa Daesh na makundi mengine ya kigaidi huko Syria yanaelekezwa katika mazungumzo muhimu ya Geneva. Mafanikio hayo ni matunda ya jitihada na mchango wa moja kwa moja wa Iran na Russia na baadaye Uturuki ambayo imeamua kujiunga na mkondo huo.
Awali Uturuki ilikuwa ikisisitiza udharura wa kuondolewa madarakani serikali ya Syria na kulitambua suala hilo kuwa ni katika fremu ya maslahi yake ya kiusalama. Hata hivyo inaonekana kuwa, Ankra imekiri kuwa ilikuwa imetumbukia katika makosa ya kimahesabu.
Kwa sasa kumejitokeza mazingira mapya kwa ajili ya ushirikiano baina ya nchi hizo jirani. Zaidi ni kwamba, misimamo ya Iran na Uturuki imekaribiana zaidi kuhusu masuala ya Iraq na hasahasa kadhia ya kuitishwa kura ya maoni juu ya eneo la Kurdistan.
Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, maudhui ya kura ya maoni kuhusu suala la kujitenga eneo la Kurdistan huko kaskazini mwa Iraq litazigonganisha nchi tatu za Iran, Uturuki na Iraq na kwa sababu hiyo viongozi wa nchi hizi mbili wanasisitiza kuwa ni jambo lisilowezekano na haliwezi kufanyika.
Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, makubaliano na mazungumzo ya viongozi wa kijeshi wa Iran na Uturuki yanalenga kuanzisha mlingano mpya katika eneo hili la Mashariki ya Kati na kukabiliana na mipango ya nchi za Magharibi. Samir Saleh ambaye ni mhadhiri wa mahusiano ya kimataifa katika Chuo Kikuu cha Istanbul nchini Uturuki anasema: "Safari ya Meja Jenerali Mohammad Baqeri na mazungumzo yake na viongozi wa Ankara ni kwa ajili ya kuweka taratibu za kukabiliana na jambo lolote linalotishia maslahi ya Iran na Uturuki kuhusu kadhia ya Syria na Iraq".