Wapalestina wawasilisha ushahidi wa jinai za Israel dhidi yao ICC
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i34635-wapalestina_wawasilisha_ushahidi_wa_jinai_za_israel_dhidi_yao_icc
Mawakili na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Palestina wamewasilisha ushahidi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inayothibitisha kuwa vyombo vya dola vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimehusika katika jinai dhidi yao.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 20, 2017 22:02 UTC
  • Wapalestina wawasilisha ushahidi wa jinai za Israel dhidi yao ICC

Mawakili na wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wa Palestina wamewasilisha ushahidi mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC inayothibitisha kuwa vyombo vya dola vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimehusika katika jinai dhidi yao.

Ushahidi huo wenye kurasa 700 unabainisha jinai, ubaguzi na mauaji dhidi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na mashariki mwa Quds Tukufu inayokaliwa kwa mabavu.

Shawan Jabarin, Mkurugenzi wa shirika la kutetea haki za binadamu la Palestina la al-Haq amesema ushahidi huo unafichua namna maafisa usalama wa Israel wanavyowafurusha Wapalestina kutoka makazi yao na ardhi zao kughusubiwa na walowezi wa Kiyahudu.

Mwezi Juni mwaka jana, shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Rights Watch liliitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ianze kuwafuatilia kisheria viongozi wa utawala wa Kizayuni wanaofanya jinai za kivita dhidi ya Wapalestina hasa wanaotekwa nyara na utawala huo, na kuitaka ICC iwapandishe kizimbani viongozi hao wa Israel.

Hali ya kusikitisha katika Ukanda wa Gaza

Miezi minne baadaye, timu ya wataalamu wa ICC ikiongozwa na Mwendesha Mashtaka Mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda, ilifanya safari katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Mojawapo ya malengo ya safari hiyo ilikuwa kuchunguza uvamizi wa kijeshi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza mwaka 2014, ambapo Wapalestina 2,200 wakiwemo watoto wadogo zaidi ya 500 waliuawa shahidi na askari katili wa Israel.