Kura ya maoni Kurdistan na namna Barzani anavyochezea moto
Katika hali ambayo kulikuwapo tetesi za kufanyika au kutofanyika kura ya maoni ya kujitenga eneo la Kurdistan la Iraq, hatimaye Masoud Barzani, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Kurdistan Iraq amesisitiza kuhusu kufanyika kura hii ya maoni leo hii.
Tarehe 7 Juni Masoud Barzani alitangaza azma ya eneo la Kurdistan la Iraq ya kuandaa kura ya maoni Septemba 25 kwa lengo la kujitenga eneo la Kurdistan.
Katika kipindi cha wiki moja iliyopita kumekuwepo na upinzani mkubwa kuhusu kura ya maoni eneo la Kurdistan. Upinzani huo ulikuwa ndani ya eneo hilo lenyewe, kote Iraq, Mashariki ya Kati na kimataifa kiasi cha Haider al Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq na baadhi ya shakhsia katika nchi zinazopakana na Iraq wametaja kura hiyo ya maoni huwa ni kucheza na moto.
Hadi Sayyed Afqahi mtaalamu wa masuala ya Mashariki ya Kati anasisitiza kuwa, Barzani anacheza na moto na kuongeza kuwa: "Rais wa eneo la Kurdistan anachezea moto ambao ni mkubwa zaidi ya uwezo wake wa kisiasa." Hapa linajitokeza swali wkamba ni nini Masoud Barzani hazimi moto huo kabla haujaibua mgogoro mpya?
Weledi wa mambo wanasema anafuatilia malengo matatu yafuatayo:
Lengo la kwanza la kuandaliwa kura ya maoni Kurdistan ni kuwa, Barazani anataka aonekane kama kiongozi bingwa wa Wakurdi na pia athibitishe kuwa, sisitizo lake la kubakia madarakani kinyume cha sheria kama rais wa eneo lenye mamlaka ya ndani ya Kurdistan, halikuwa bila sababu. Barzani alitakiwa kuondoka madarakani miaka minne iliyopita. Kwa hivyo anataka kubakia katika historia ya Wakurdi kama mtu aliyeitisha kura ya maoni ya kujitenga eneo hilo na Iraq.

Lengo la pili la Barzani katika kura ya maoni ya eneo la Kurdistan ya Iraq ni kuwafanya Wakurdi wawe kaumu ambayo inayotaka serikali kuu ya Iraq itekeleze matakwa yake. Kwa maneneo mengine ni kuwa, Barzani anataka kuonyesha kuwa, ile dhana ya kujitenga imepata nguvu miongoni mwa Wakurdi. Hata kama matokeo ya kura ya maoni Kurdistan yatakuwa chanya, lakini hayawezi kuhesabiwa kuwa ni haki, kwani eneo hilo ni sehemu ya ardhi ya Iraq, na dunia ina maeneo mengi yenye matatizo ya kikaumu ambayo hayawezi kutatuliwa kwa kujitenga. Iwapo mkondo huo utafuatwa, nchi nyingi duniani zitakabiliwa na tatizo la maeneo yanayotaka kujitenga na kwa msingi huo jamii ya kimataifa inapinga eneo la Kurdistan kujitenga. Ni kwa msingi huo ndiyo maana weledi wa mambo wanatahadharisha kuhusu athari mbaya za kura ya maoni ya Kurdistan kwa maeneo mengine duniani.
Lengo la tatu muhimu la Masoud Barzani katika kuitisha kura ya maoni huko Kurdistan, ni kuwaweka katika mtihani viongozi wa kitaifa na kieneo. Inaelekea kuwa, Masoud Barzani hakuzipatia uzito tahadhari na indhari za kitaifa na kikanda na hivyo anataka kuona iwapo waliotoa vitisho watatekeleza vitisho vyao au la.
Iwapo vitisho hivyo vitatekelezwa kivitendo au kama kutashuhudiwa umwagikaji mkubwa wa damu, basi Masoud Barzani atakuwa muathirika wa kwanza. Aidha nchi za kanda hiyo kama Uturuki, Iran na Syria zinaweza kutoa radiamali isiyo ya kivita lakini ambayo itakuwa na madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii kwa Kurdistan. Iwapo vitisho vya awali havitatekelezwa na Kurdistan ikafuata mkondo rahisi wa kujitenga na Iraq, basi Barzani atakuwa amefikia lengo lake kuu la kuwa bingwa shujaa wa Wakurdi.
Hata hivyo ni jambo lililo mbali sana kwa Iraq na nchi za kanda hii kuiacha Kurdistan ijitenge itakavyo. Kwa hivyo kuwajaribu viognozi wa nchi za eneo hilo na duniani ni sera isiyo na busara kwani inaweza kupelekea kuibuka umwagikaji wa damu na matatizo mengi ya kijamii na kiuchumi.